Hivi punde: Tamko la Mheshimiwa Sayyid Sistani baada ya kumpokea muwakilishi wa umoja wa mataifa Jumapili ya leo

Maoni katika picha
Mheshimiwa Ayatullah Mkuu Sayyid Sistani kabla ya Adhuhuri ya leo amempokea bibi Jenin Haines, muwakilishi maalum wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa hapa Iraq, Mheshimiwa akasema msimamo wake katika baadhi ya mambo muhimu, kama ifuatavyo:

Kwanza: Hakika uchaguzi wa bunge unaotarajiwa kufanyika mwakani unaumuhimu mkubwa, inatakiwa ziundiwe kanuni zitakazo wezesha kuwa na uchaguzi huru na wa haki pamoja na kuwafanya wananchi washiriki kwa wingi, hivyo lazima ufanyike kwa misingi ya haki na uwadilifu bila kujali maslahi ya baadhi ya vikundi na vyama vya kisiasa, lazima haki izingatiwe katika ngazi zote, usimamiwe vizuri na watu waliobobea katika mambo ya uchaguzi wakiwemo wajumbe wa umoja wa mataifa.

Kufanya uchaguzi wa mapema sio lengo peke yake, bali ni njia sahihi ya kuondoka katika hali inayo likumba taifa kwa sasa, katika sekta ya siasa, uchumi, amani, afya nk.. lazima wananchi wapewe nafasi ya kuchagua bunge lijalo kwa uhuru na amani, bila kushurutishwa na yeyote, na bunge hilo litatue matatizo ya wananchi. Kuendelea kuchelewa kufanya uchaguzi au kufanya bila kufuata taratibu za uchaguzi huru na wa haki, kwa namna ambayo matokeo yake hayatakubaliwa na sehemu kubwa ya raia kutaongeza matatizo ya taifa –Allah atuepushie- na kutishia mustakbali wa nchi, kila mtu atajuta mambo yatakapo haribika.

Pili: Hakika serikali iliyopo inatakiwa kuendeleza utulivu na kufanya uadilifu, pamoja na kulinda mipaka na kuboresha vyombo vya ulinzi na usalama, sambamba na kuchukua siraha ambazo zipo mikononi mwa watu kinyume na sheria, wala isikubali baadhi ya maeneo kutawaliwa na makundi yenye siraha kwa mtutu wa bunduki chini ya visingizio mbalimbali kinyume na sheria.

Serikali inatakiwa kuchukua hatua madhubuti za kupambana na ufisadi kwa mujibu wa sheria, kila mtu aliye fanya ufisadi ahukumiwe kisheria na arudishe mali za wananchi bila kujali nafasi yake au chama chake.

Aidha inawajibika kumchukulia hatua kila aliyeshiriki katika jinai ya kuuwa au kujeruhi au kufanya shambulio lolote kwa waandamanaji au vyombo vya ulinzi na usalama, au aliharibu mali za umma au binafsi, tangu lilipo anza vuguvugu la kudai mabadiliko (islahi) mwaka jana, hususan wale waliofanya vitendo vya utekaji na mashambulio mengine.

Hakika kuwachukulia hatua watu waliofanya makosa tuliyo taja ni jambo linalotakiwa kufanyika siku yeyote, ni njia sahihi ya kuzuwia jambo hilo lisirudiwe tena na kuogopesha watu wengine kufanya hivyo.

Tatu: Kulinda heshima ya taifa na kuzuwia kuingiliwa na ushawishi wa kutoka nje ya taifa katika mambo ya ndani ya nchi na kuzuwia mpasuko wa taifa ni jukumu la kila mtu, ni jambo la kizalendo na kulinda maslahi ya wairaq sasa na baadae, jambo hilo haliwezi kufanikiwa kama watu wataweka mbele maslahi binafsi, ya chama au eneo, ni jukumu la kila mtu kuweka mbele maslahi ya taifa na kujiepusha na jambo lolote linalo vunja amani na utulivu.
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: