Marjaa dini mkuu awataka wafanya ziara wenye kushiriki katika kuhuisha Usiku wa Nusu ya Shaaban, kuwakumbuka ndugu zao wapiganaji ambao kama si mihanga yao wanayojitolea basi furaha ya wafanya ziara hao ingekuwa huzuni..

Maoni katika picha
Marjaa dini mkuu kupitia mwakilishi wake Mheshimiwa Sheikh Abdulmahadi Karbalaiy, amewataka wafanya ziara wanaoshiriki katika kuhuisha usiku wa nusu ya Shaaban, katika kukumbuka mazazi ya Imam Mahdi Mwenye kungojewa, Allah aharakishe faraja yake, wawakumbuke ndugu zao wanaopigana katika medani za vita, ambao kama si mihanga yao wanayojitolea basi furaha ya wafanya ziara hao ingekuwa huzuni. Hivyo amewataka watenge sehemu ya hotuba zao na kaswida zao kwa ajili ya kusifu ushujaa wao, na waeleze umuhimu wa kuendeleza safari yao katika kujitolea muhanga na fidia, mpaka ukamilike ushindi wa mwisho kwa msaada Wake Mtukuka. Maelezo hayo yamekuja katika hotuba ya pili ya Swala ya Ijumaa ya mwezi 8 Shaaban 1438 Hijiriya, sawa na tarehe 5 Mei 2017 Miladiya, Swala iliyoswaliwa katika ukumbi wa haram ya imamu Hussein (a.s) chini ya uimamu wa Sheikh Karbalaiy, ambapo Mhesimiwa alisema:

Ndugu zangu mabibi na mabwana, napenda kubainisha kwenu na kuwasilisha masikioni mwenu jambo lifuatalo: Usiku wa Ijumaa ijayo – Usiku wa Nusu ya Shabaan muadhamu – utakutana na utukufu wa usiku utokanao na ibada, dua na tahajudi kwa ajili ya Allah, kwa kukumbuka kuzaliwa kwa Hoja mwana wa Hassan Mwenye kungojewa, Allah aharakishe faraja yake tukufu. Nao ni mnasaba adhimu ambao ndani yake wapenzi wa Ahlulbayti (as) huonesha furaha yao kupitia mazazi hayo. Na wengi miongoni mwao watakuja hapa Karbala Tukufu kumzuru Imamu Hussein (as). Aidha kuna mnasaba mwingine ulio mzito juu ya nyoyo zetu sote, nao ni kukumbuka wito wa Marjaa Mkuu wa Kidini alioutoa katika siku ya mwezi kumi na nne Shaaban 1435 Hijiriya, yaani miaka mitatu iliyopita, wa kuwataka wale wenye uwezo wa kubeba silaha, kujiunga na vikosi vyenye silaha kwa ajili ya kuitetea ardhi ya Iraq, raia wake na matukufu yake, mbele na dhidi ya mashambulizi ya makundi ya uovu ya DAESH. Na hatimaye maelfu ya vijana na wazee waliitikia wito huo na wakatekeleza jukumu hili adhimu. Na hatuna budi hapa kutaja mambo mawili:

Jambo la Kwanza: Tunatoa shukurani, heshima na taadhima kwa wapendwa wetu wenaopigana katika vikosi vya kupambana na ugaidi, na wale waliopo katika kikosi cha ulinzi wa haraka, na katika jeshi kwa ujumla wa vikosi vyake vyote, na askari wa muungano, na waliopo katika makundi ya wanamgambo wa kujitolea kwa majina yake yote. Tunatoa shukurani, heshima na taadhima kwa mihanga mikubwa waliyojitolea, na kwa damu safi waliyojitolea, na kwa mapambano makubwa ya kizalendo waliyoyatoa kwa ajili ya kuihami Iraki na kuisafisha na uchafu wa ugaidi wa DAESH. Na wakati wakiwa wanaendelea kuyakomboa maeneo yaliyobakia ya Mkoa wa Naynawa katika siku hizi, tunatoa wito wa kuongezwa mshikamano na kusaidiana baina ya vikosi vyenye kushiriki katika mapambano, ili kwa haraka sana zifunikwe kurasa za mwisho za kuukomboa mkoa azizi ambao ulitoa thamani kubwa mbele ya makundi ya ugaidi. Hakika sisi tunajua kwamba hakika wao wanatoa mihanga mikubwa katika njia ya kulinda kwa kadiri iwezekanavyo roho za raia wa maeneo hayo, ambao makundi ya DAESH yaliwafanya ngao za kivita. Lakini pia ni ili watambue kwamba mihanga hii ghali haitapotea bure bali itajenga msingi imara ya umoja wa nchi hii, ardhi hii na taifa hili, inshaallah.

Jambo la Pili: Tunapenda kugeuza mitazamo ya wenye kusheherekea mnasaba huu wa mazazi haya matukufu katika nusu ya Shaaban, kwamba hakika vita hivi vya hatima yetu ambavyo taifa letu na wapiganaji wa vikosi vyenye silaha na wanamgambo mashujaa wa kujitolea wameviingia, vimewadondosha mashahidi wengi na kuwaacha wengi wakiwa majeruhi. Aidha vimetuachia ongezeko la wajane na mayatima, na vimepelekea idadi kubwa ya raia kukimbilia nje ya miji yao na vijiji vyao. Na kuanzia hapa ni lazima hali ya furaha na sururi katika hafla hizi ambazo zinafanywa katika mnasaba huu, iwe ndani ya mipaka inayooana na mazingira maalumu yaliyojitokeza na yanayopitiwa na nchi yetu. Kama ambavyo inapasa kwa wanaoshiriki hafla hizi kutowasahau katika hafla hizi ndugu zao wanaopambana katika medani za vita, ambao kama si mihanga yao wanayojitolea basi furaha yao ingekuwa huzuni. Hivyo watenge sehemu ya hotuba zao na kaswida zao kwa ajili ya kusifu ushujaa wao, na waeleze umuhimu wa kuendeleza safari yao katika kujitolea muhanga na fidia, mpaka utimie ushindi wa mwisho kwa msaada Wake Mtukuka. Kama ambavyo inapasa kwa wote kutumia sehemu ya thamani zao na uwezo wao katika kuwaunga mkono wapiganaji waliopo katika medani za vita, na kutoa huduma kwa wanaokimbia mapigano, mayatima na wajane. Na wajitume katika kufanya amali za ziada zitakazowaweka karibu na Allah Mtukuka.

Tunamuomba Allah Mtukuka atuafikishe katika hayo, na ayapokee hayo kutoka kwetu kwa mapokezi mazuri. Na atupe ushindi wa haraka, wenye nguvu na usiyokwisha, hakika Yeye ni Msikivu na Mwenye kujibu. Na kila sifa njema ni ya Allah Mola Mlezi wa walimwengu. Na sala za Allah ziwe juu ya Muhammad na juu ya Aali zake wema watoharifu.
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: