Usiku wa Arafa: Ni usiku mtukufu sana na huitwa usiku wa kuomba na kukidhiwa haja, toba hukubaliwa katika usiku huo na dua hupokelewa, mwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu katika usiku huo huandikiwa thawabu za kufanya ibada miaka sabini, katika usiku huu kuna ibada nyingi za kufanya:
Kwanza: Asome dua isemayo: (Allahumma yaa shaahida kulli najwa, wa maudhia kulli shakwa, wa aalima killi khafiyya…) imepokewa kuwa atakaye soma dua hiyo katika usiku wa Arafa au usiku wa Ijumaa Mwenyezi Mungu atamsamehe. Angalia katika ibada za siku ya Arafa katika kitabu cha Mafaatihul jinaani.
Pili: asome tasbihaati kumi mara elfu moja zilizo pokewa na Sayyid ibun Twawuusi: (Subhana Llahi qabla kulli ahad, Subhana Llahi ba’ada kulli ahad…). Angalia katika ibaza za siku ya tisa katika mwezi wa Dhulhijja / Mafaatihul jinaani.
Tatu: Asome dua isemayo: (Allahumma man ta’abba-a wa tahayya-a…) ambayo imesuniwa kusomwa katika siku ya Arafa na usiku wa Ijumaa na mchana wake. Angalia ibada za siku ya Ijumaa / Mafaatihul jinaani.
Nne: Amzuru Imamu Hussein (a.s) na ardhi ya Karbala, na abakie katika ardhi ya Karbala hadi siku ya Idi, ili Mwenyezi Mungu amuepushe na shari za mwaka huo.
Siku ya Arafa: Ni Idi miongoni mwa Idi kubwa, japokua haijulikani kama ni siku ya Idi, hakika ni siku ya furaha, ni siku ambayo Mwenyezi Mungu mtukufu amewataka waja wake wamtii na kumuabudu, na amewafungulia milango ya mbingu zake, ili waumini wapate ladha ya kumuomba, hilo peke yake latosha kua siku ya furaha kwa waumini kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu mtukufu anasema: (Na mtakapo miminika kutoka Arafa mtajeni Mwenyezi Mungu penye Mash’aril Haram..) surat Baqara: aya ya 198. Mwenyezi Mungu amewawekea ihsaani yake na utukufu wake, na amewaahidi kuwasamehe madhambi na kuwasitiri aibu zao pamoja na kufariji nyoyo zao, na ameruhusu kuombwa na kila mtu mwenye kujikurubisha kwake na asiye jikurubisha, shetani katika siku hiyo ni dhalili mnyonge anahasira kushinda wakati wowote ule, siku hii inaibada nyingi:
Kwanza: Kuoga.
Pili: Kufunga kwa yule ambaye funga yake haitamfanya ashindwe kufanya ibada za siku hii tukufu.
Tatu: Kumzuru Hussein (a.s), ni sawa na hijja elfu moja na umra elfu moja na kupigana jihadi bali ni zaidi ya tulivyo taja, hadithi kuhusu utukufu wa kumzuru (a.s) katika siku hii ni mutawatira, atakaye weza kumzuru (a.s) na kusimama chini ya kubba lake tukufu thawabu zake ni sawa na aliye simama Arafa bali anamzidi, Imamu Swadiq (a.s) anasema: (Hakika Mwenyezi Mungu mtukufu huelekea kwa mazuwaru wa kaburi la Hussein (a.s) kabla ya kuelekea Arafa, na huwakidhia haja zao, na kusamehe dhambi zao, na kuwapokelea maombi yao, kisha anaelekea Arafa na kuwafanyia kama alivyo wafanyia hawa).
Nne: Baada ya swala ya Alasiri na kabla ya kuanza kusoma dua za Arafa, swali rakaa mbili chini ya mbingu na ukiri dhambi zako, ili upate thawabu za Arafa na usamehewe dhambi zako, ni vizuri ukasoma (Alhamdu) na (Tauhiid) katika rakaa ya kwanza, na katika rakaa ya pili usome (Alhamdu) na (Qul-yaa-ayyuhal kaafiruun), kisha ndio uanze kusoma dua za Arafa kama zilivyo elekezwa na Maimamu watakasifu (a.s), nazo ni nyingi sana hatuwezi kuzitaja zote, tumeandika baadhi yake tu.
Tano: Baada ya hapo swali rakaa nne kwa salamu mbili, katika kila rakaa usome (Alhamdu) mara moja na (Tauhiid) mara hamsini, nayo ni swala ya Kiongozi wa Waumini (a.s).
Sita: Usome dua iliyo tajwa na Sayyid ibun Twawuusi katika kitabu cha Iqbaal ambayo imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) isemayo: (Subhaana lladhii fii samaai a’rshuhu, Subhaana lladhii fil-ardhi hukmuhu…). Angalia ibada za siku ya tisa Dhulhijja / Mafaatihul Jinaani.
Saba: Usome dua hii, imepokewa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s): Atakaye taka kumfurahisha Muhammad na Aali Muhammad awatakie rehma kwa kusema: (Allahumma yaa Ajwada man a’atwaa, wa yaa khaira man suila, wa yaa arhama manisturhima, Allahumma swalli alaa Muhammadi wa Aalihi fil-awwaliin…). Angalia ibada za siku ya tisa Dhulhijja / Mafaatihul Jinaani.
Nane: Usome dua ya Ummu Daudi iliyo tajwa katika ibada za mwezi wa Rajabu, kisha asome tasbihi isemayo (Subhana Llahi qabla kulli ahad, Subhana Llahi ba’ada kulli ahad…). Angalia ibada za siku ya tisa Dhulhijja / Mafaatihul Jinaani.
Tisa: Kusoma dua ya Imamu Hussein (a.s) katika siku ya Arafa.
Kuna dua na ibada nyingi katika siku hii tukufu kwa aliye fanikiwa kufika katika viwanja vya Arafa, na ibada bora zaidi ya siku hii ni kusoma dua, ni siku tukufu sana kwa kuomba dua, na inafaa kuwaombea ndugu zetu waumini walio hai na walio kufa.