Shangwe na furaha imejaa katika nyumba ya Imamu Mussa bun Jafari (a.s), katika siku kama ya leo mwezi kumi na moja Dhulqaada mwaka (148) hijiriyya kwenye mji wa Madina, alizaliwa mwanae Imamu Ali Ridhwa (a.s), Imamu wa nane katika orodha ya Maimamu watakasifu (a.s).
Ardhi imeng’aa kwa kuzaliwa Imamu Ridhwa (a.s), furaha imejaa kwa watu wa nyumba ya Mtume (a.s), Imamu Mussa Alkadhim alipokea taarifa hiyo kwa furaha kubwa, akaenda haraka kwa mke wake na kumpongeza, akasema: (Hongera sana ewe nyota Mwenyezi Mungu amekukirim..).
Riwaya zinaonyesha kuwa Imamu Alkadhim (a.s) alimchukua mtoto wake mtukufu akiwa amefunikwa kitambaa cheupe, akamuadhinia kwenye sikio la kulia na kumsomea iqama kwenye sikio la kushoto, akamuwekea mdomoni maji ya mto Furaat, kisha akamrudisha kwa mama yake, akasema: (Mchukue hakika huyu ni hoja ya Mwenyezi Mungu katika ardhi yake..).
Imamu Ridhwa (a.s) amekulia ndani ya nyumba tukufu zaidi katika uislamu, nyumba ya Uimamu na wahyi, nyumba ambayo Mwenyezi Mungu aliamuru ijengwe na litajwe jina lake humo, hakika alipata malezi bora kabisa ya kiislamu, alikua anamheshimu mdogo na kumhurumia mkubwa, alikua na adabu sana mwenye tabia bora, muda wote alikua anasoma kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kuhimiza matendo mema yanayo mkurubisha mja kwa Mola wake.
Kuzaliwa kwake (a.s) ulikua muendelezo wa kheri, uongofu na tauhidi, hakika alikua (a.s) kiongozi wa kiroho, Imamu wa nane katika Maimamu wa nyumba ya Mtume (a.s) watakasifu, amani iwe juu yake siku aliyozaliwa na siku aliyouawa kwa sumu na siku atakayo fufuliwa kuwa hai na kutoa Ushahidi kwa umma.