Muwakilishi wa Marjaa Dini mkuu Mheshimiwa Sayyid Ahmadi Swafi siku ya Ijumaa ya mwezi (24 Rajabu 1441h) sawa na (20 Machi 2020m) ametoa ujumbe elekezi kuhusu maambikizi ya virusi vya Korona duniani.
Ufuatao ni ujumbe wa tamko hilo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Abul-Qassim Muhammad na Aali zake watakasifu.
Mwenyezi Mungu ayakuze malipo yenu kwa kifo cha Imamu Mussa bun Jafari (a.s) ambae kumbukumbu ya kifo chake itakua kesho siku ya Jumamosi, tunamuomba Mwenyezi Mungu atuondeshee balaa na atupe amani daima kwa utukufu wa Muhammad na Aali wate watakasifu.
Amani iwe juu yenu mabwana na mabibi katika siku hii tukufu –siku ya Jumaa- tunamuomba Mwenyezi Mungu mtukufu adumishe taufiq.
Napenda nizungumze nukta tatu, kwanza nukta ya Dini, pili nukta ya tiba na tatu ya kijamii.
Sababu ya kuongea kwangu kama mnavyo fahamu, taifa letu na mataifa mengine duniani yanatatizo la maambukizi ya virusi vya Korona, tunamuomba Mwenyezi Mungu atuepushie balaa hilo, wiki mbili zilizo pita tuliongea kuhusu Dini, leo nitazungumza nukta hiyo kidogo halafu niingie katika nukta zingine mbili.
Mnatambua kua Mwenyezi Mungu mtukufu, kwa mujibu wa itikadi yetu anasema (Sema hatutapatwa na jambo ispokua alilotuandikia Mwenyezi Mungu), Muumini wakati woto huwa anautulivu, huo ndio uhusiano kati ya mja na Mola wake, kama ilivyo pokewa katika baadhi za dua (Kheri yako hushuka kwetu na shari zetu hupanda kwako), tunaamiliana na Mwenyezi Mungu mtukufu, naye ndio kilele cha kheri na rehema, kila kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu mja anatakiwa akiheshimu na kukinyenyekea, kawaida mwanadamu hutoka katika hali moja hadi nyingine, ndio.. mwanaadamu anatakiwa alinde nafsi yake, pia tunaamini kua sheria imehimiza jambo hilo, hairuhusu kuangamiza nafsi zetu, bali ni wajibu kuzilinda, hata katika tatizo hili (Korona) hatutakiwi kudharau, tuchukue tahadhari zote zinazo takiwa katika kulinda nafsi zetu –Allah atuepushie- sio kulinda nafsi yako tu, bali unatakiwa kulinda nafsi za watu wengine pia, kwa kufuata maelekezo yanayo tolewa na idara za afya, kwa hiyo lengo ni kulinda nafsi zetu na za watu wengine pia, jambo hilo halipingani na mtazamo wa kwanza, mwanaadamu hukabidhi kila jambo kwa Mwenyezi Mungu mtukufu, lakini wakati huohuo mafundisho ya Mwenyezi Mungu yanatutaka kuzilinda nafsi zetu, tunatakiwa kuchukua tahadhari kwa ajili ya kulinda nafsi zetu, tunamuomba Mwenyezi Mungu atulinde na balaa hili, naona niishie hapa katika nukta hii.
Nukta ya pili ni maswala ya tiba, siku nne zilizo pita, ilikua mwezi (21 Rajabu) kuna maswali yalielekezwa kwa Mheshimiwa Sayyid Sistani, mimi nataja nakala hiyo ambayo hata nyie mnaitambua, nitaeleza baadhi ya vipengele, tunstakiwa kuheshimu sekta ya madaktari, angalieni maneno aliyotumia Mheshimiwa Sayyid alipo taja sekta hii, alisema: (Hakika kutibu wagonjwa na kuwahudumia ni wajibu kifaya) maana ya wajibu kifaya ni kwamba lazima wapatikane watu watakao fanya kazi hiyo, ni watu gani hao? Akasema: (Kwa kila mwenye uwezo wa kufanya hivyo), kawaida wenye uwezo na jambo hilo ni madaktari na wauguzi, pamoja na wasaidizi wao katika kuhudumia wagonjwa, hali kadhalika lazima wapewe vitendea kazi, ndipo Mheshimiwa akasema: (Ni wajibu kwa wenye mamlaka…) akimaanisha waliopo katika ngazi za maamuzi wanalazimika kufanya nini? (wanalazimika kuandaa vifaa vyote vinavyo hitajika katika kutekeleza jukumu hilo), akasisitiza kua: (wala hawapaswi kutoa udhuru wa kutofanya jambo hilo), angalieni jambo hilo, kisha akafananisha kazi wanazo fanya mdaktari na wauguzi na kazi inayo fanywa na wapiganaji kwenye uwanja wa vita, wanapo pigana na aduwi wa wazi (Daesh) au magaidi wengine, wapiganaji huwazuwia magaidi hao wasidhuru watu na taifa, madaktari na wauguzi pia wanapambana kuzuwia maradhi yasiangamize watu, kwa hiyo inatarajiwa kuwa thawabu zao zinafanana na thawabu za majemedari hawa, -Allah atuepushie- ikitokea mmoja wao kafa kwa sababu ya kumuhudumia mgonjwa ataandikiwa thawabu sawa na shahidi, kwa hiyo tupo mbele ya jambo muhimu yatupasa tuwe na mazingatio, kama nilivyo sema; mtazamo wa Dini unamtaka kila mtu awe na utulivu, lakini pia mtazamo huohuo wa Dini unakutaka ulinde nafsi yako, usiingize nafsi yako katika maangamizi, tunatakiwa kusikiliza na kufuata maelekezo yanayo tolewa na idara za afya, kwani tusipo fanya hivyo tunaweza kudumbukia katika hatari kubwa, mnajua wazi kila siku tunapewa orodha mpya ya maambukizi ya virusi hivi (Korona), kuna nchi zinadai kua zimeendelea katika mambo ya tiba lakini virusi hivyo vinasambaa kwa kasi katika nchi hizo, mtu anaefuatilia taarifa za kidaktari anatambua ukubwa wa tatizo, idara za afya kote duniani zimetoa maelekezo kulingana na uwezo wa kila taifa.
Kwa hiyo ndugu zangu hatutakiwi kudharau mambo haya, yatupasa kufanyia kazi maelekezo tunayo pewa, kwa kuhofia mambo yasiharibike, Mwenyezi Mungu hakuruhusu kuangamiza nafsi zetu, mwanaadamu anatakiwa afanye mambo kwa elimu, wataalamu wanapo gundua kitu na kutoa tahadhari lazima tuwasikilize hadi balaa hili litakapoisha, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mataifa mbalimbali yapate amani.
Nukta ya tatu ninayo penda kuongea ni mambo ya kijamii, nyie mnajua kua mambo ya kijamii yanayo kusudiwa na kusaidiana baina yetu, kuoneana huruma ni miongoni mwa sifa nzuri kwa mila zote na Dini zote, watu wanatakiwa kusaidiana, kufanyiana mambo mema, kila mmoja amsaidia mwenzake, watu hawatakiwi kutumia balaa hili kwa kujinufaisha wenyewe, kuna baadhi ya watu waovu walitaka kujinufaisha kupitia balaa hili, watu watakapo hurumiana na kusaidiana inaweza kuwa sababu ya Mwenyezi Mungu kuwahurumia na kuondoa balaa hili, lakini tutakapozuwia misaada au tukaongeza bei za bidhaa tutawapa uzito zaidi hususan watu wenye kipato cha chini, naamini wote mtakubaliana na mimi kufanya hivyo sio vizuri, ndugu zangu tupo katika wakati ambao tunahitaji kusaidiana zaidi, aidha tunapongeza kuzi kubwa inayo fanywa na madaktari pamoja na wauguzi wanao hangaika usiku na mchana kupambana na maradhi haya, wakati huohuo tunatakiwa kuweka mazingira mazuri yatakayo mpa matumaini mgonjwa, katika nchi nyingi kuna idadi kubwa ya watu walio ambukizwa virusi vya Korona na hali zao zinaendelea vizuri, tunatakiwa kuendelea kujikinga hadi tutakapo vuka kipindi hiki kigumu, hatupaswi kutiana hofu kubwa wala kudharau tunatakiwa kuwa makini na kuchukua tahadhari, huenda Mwenyezi Mungu mtukufu atatuondolea balaa hili, tunamuomba atupe amani.
Na mwisho wa maombi yetu husema kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu, na rehma zake ziwe juu ya Muhammad na Aali wake watakasifu.