Katika siku kama ya leo, mwezi kumi na moja Dhulqaada mwaka wa (148) hijiriyya katika mji wa Madina, nyumba ya Imamu Mussa bun Jafari (a.s) ilijaa furaha kwa kuzaliwa Imamu Ali bun Mussa Ridhwa (a.s), naye ni Imamu wa nane katika orodha ya Maimamu watakasifu (a.s).
Ardhi ilinawirika kwa kuzaliwa Imamu Ridhwa (a.s), hakika amezaliwa mbora wa viumbe wa ardhini, na mwingi wa kurejea kwenye uislamu, wingu la furaha limetanda kwa watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w), Imamu Kadhim (a.s) alipokea taarifa ya kuzaliwa mtoto huyu kwa furaha kubwa, akaenda haraka kumpongeza mke wake, akasema: (Hongera sana ewe Najma Mola wako amekukirimu..) akambeba mtoto mtakatifu akiwa amefungwa kwenye kitambaa cheupe, akamuadhinia kwenye sikio la kulia na akamkimia kwenye sikio la kushoto, akachukua maji ya mto Furaat akamuwekea mdomoni kisha akamrudisha kwa mama yake, akasema: (Mchukue hakika huyu ni Baqiyyatu-Llahi katika ardhi yake..).
Imamu Ridhwa (a.s) alilelewa kwenye nyumba tukufu zaidi katika uislamu, nyumba ya Imamu, ambayo ni miongoni mwa nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe na litajwe jina lake ndani ya nyumba hizo, alilelewa Imamu ndani ya nyumba hiyo tukufu na akapewa malezi bora ya usiamu, alikua anamsheshimu mdogo na kumhurumia mkubwa, naye mkubwa anamuonea huruma mdogo, nyumba iliyojaa adabu na ukarimu, sauti inayo sikika ndani ya nyumba hiyo ni sauti ya usomaji wa Quráni na kuhimizana kufana mema na mambo yanayo mkurubisha mja kwa Mola wake.
Kuzaliwa kwake (a.s) kulichochea kufanya mema na tauhidi, alikuwa (a.s) ni kiongozi wa kiroho muokozi wa waja kwenye kimbunga cha matamanio na uovu, ni Imamu wa nane katika Maimamu wa nyumba ya Mtume watakasifu (a.s), amani iwe juu yake siku aliyo zaliwa na siku aliyo uwawa kwa sumu na siku atakayo fufuliwa kuwa hai na kutoa ushahidi kwa umma.