Waziri wa afya na mazingira nchini Iraq Dokta Hassan Muhammad Tamimi amepongeza kazi zinazo fanywa na Atabatu Abbasiyya tukufu, kwa kusaidia wizara yake katika mji wa Bagdad na mikoa mingine kupambana na janga la Korona, kupitia miradi ya kusaidia sekta ya afya inayo fanywa na Ataba hiyo.
Hayo yamesemwa katika msafara wa waziri pamoja na mganga mkuu wa Bagdad Dokta Abdughina Saaidiy pamoja na watumishi wa wizara, baada ya kuangalia mradi wa ujenzi wa kituo cha kuhudumia watu walio ambukizwa virusi vya Korona, unaofanywa na Atabatu Abbasiyya tukufu katika hospitali ya Ibun Qafi kitongoji cha Raswafa mjini Bagdad, siku ya Alkhamisi mwezi (17 Dhulqaada 1441h) sawa na tarehe (7 Julai 2020m).
Waziri amesema kuwa: “Leo tumetembelea jengo la Alhayaat la tano, linalo jengwa na Atabatu Abbasiyya tukufu kama sehemu ya msaada wake wa kibinaadamu katika kupambana na janga la Korona, jengo hili litahudumia sehemu kubwa na litapunguza mzigo kwenye vituo vingine hapa Bagdad, tumeona jinsi wanavyo pambana ili wamalize haraka pamoja na kuweka vifaa tiba vyote vinavyo hitajika”.
Akaongeza kuwa: “Tunapongeza kazi nzuri inayo fanywa na Atabatu Abbasiyya tukufu chini ya kiongozi wake mkuu Mheshimiwa Sayyid Ahmad Swafi, ya kuisaidia wizara ya afya na madaktari katika kupambana na janga hili hususan kwenye kitongoji cha Raswafa, kama mnavyo jua kitongoji hiki ni kikubwa na kina wakazi wengi, pia kilianza kushuhudia ongezeko la maambukizi, kituo kinacho jengwa, kitasaidia kutoa huduma kwa wagonjwa wa Korona na kinatarajiwa kuanza kazi siku chache zijazo, tunamuomba Mwenyezi Mungu awawezeshe watendaji wa mradi huu ambao wanafanya kila wawezalo kukamilisha ujenzi huo ndani ya muda uliopangwa”.
Dokta Hassan Tamimi amesikiliza maelezo kutoka kwa wasimamizi wa mradi huo, ambao wamemwambia hatua za ujenzi na kiwango cha ukamilifu.
Kumbuka kuwa kituo cha Alhayaat cha tano kinajengwa kwenye kiwanja chenye ukubwa wa mita (5000), kitakuwa na vyumba (118) vya wagonjwa pamoja na vyumba ishirini vya madaktari na wauguzi, nacho ni miongoni mwa vituo vitatu vinavyo jengwa na kitengo cha usimamizi wa kihandisi cha Atabatu Abbasiyya tukufu, kwenye mkoa wa Bagdad, Muthanna na Karbala, pia nimuendelezo wa vituo vingine vitatu vilivyo jengwa katika mji wa Imamu Hussein (a.s) na katika hospitali ya Hindiyya mkoani Karbala huku kituo cha tatu kikijengwa kwa ufadhili wa hospitali ya kiongozi wa waumini (a.s) katika mkoa wa Najafu.