Mwezi saba Dhulhijjah ni kumbukumbu ya kifo cha Imamu Baaqir (a.s)

Maoni katika picha
Katika siku kama ya leo mwezi saba Dhulhijjah mwaka wa (114) hijiriyya, nyumba ya Mtume (s.a.w.w) ilipata msiba kwa kuondokewa na kipenzi wao Imamu Muhammad Albaaqir (a.s) Imamu wa tano katika Maimamu wa nyumba ya Mtume walio takaswa na kutajwa na Mtume (s.a.w.w) kuwa watakuwa viongozi baada yake.

Kwa mujibu wa riwaya ya Shekh Abbasi Qummiy katika kitabu cha Anwaru Bahiyyah fi Tawarikhi hujaju Ilahiyya inasema: Abu Jafari Muhammad bun Ali bun Hussein (a.s) aliuwawa katika mji wa Madina siku ya Jumatatu mwezi saba Dhulhijjah mwaka wa (114h) akiwa na umri wa miaka hamsini na saba.

Inasemekana alipewa sumu na Ibrahim bun Walidi bun Abdulmaliki, akafa katika siku za uongozi wa Hisham bun Abdulmaliki, Imamu Swadiq (a.s) akasimamia mazishi ya baba yake (a.s), jeneza lake lilishindikizwa na watu wengi sana, likapelekwa katika makaburi ya Baqii mjini Madini, akazikwa karibu na kaburi la Ammi wa baba yake Imamu Hassan Almujtaba (a.s), karibu na kaburi la baba yake Imamu Ali Zainul-Aabidina (a.s), alimuachia usia mwanae Jafari (a.s) usemao kuwa; amvishe sanda ya shuka aliyokuwa anaswalia siku za Ijumaa na amvishe kilemba alichokuwa anavaa, asawazishe kaburi lake na kuliinua urefu wa vidole vinne.

Imepokewa kutoka kwa Abu Abdillahi Swadiq (a.s) anasema: Baba yangu aliandika katika usia wake kuwa, sanda yake itakuwa ya shuka tatu, ya kwanza ni shuka yake aliyokuwa akiswalia siku za Ijumaa, na nyingine ni kanzu na kitambaa, nikamuambia baba: kwa nini umeandika usia huu? Akasema: naogopa watu wasikushinde. Watakaposema sanda iwe na shuka nne au tano usikubali, unifunge kilemba ambacho hakichukuliwi kuwa katika sanda, kilemba cha kawaida wanacho vaa watu wazima.

Kutoka kwake (a.s) pia anasema: Baba aliniambia: Ewe Jafari weka wakfu mali zangu kadha na kadha.

Imepokewa kuwa alihusia kuhusu dirham mia nane, jambo hilo lilipokewa katika sunna kuwa Mtume (s.a.w.w) alisema: wapeni Aali Jafari chakula hakika wameshughulishwa.

Jambo kubwa aliloshughulika nalo Abu Jafari (a.s) lilikuwa ni kusambaza elimu kwa watu, alifundisha Fiqhi na fani mbalimbali kwa watu wengi, wanafunzi wake walipata elimu kubwa na wakawa fahari ya umma huu, alimuambia mwanae Imamu Swadiq (a.s) awape chakula hadi wamalize kuandika hadithi walizo sikia kutoka kwake, nao ni katika wanachuoni bora walio hitimu kwake pia ni marafiki wakubwa wa Maimamu (a.s), Imamu Swadiq (a.s) amewasifu kwa kusema: wafuasi wa baba walikua bora zaidi yenu, walikuwa ni karatasi isiyokua na doa.

Ulimwengu wa kiislamu ulitegemea kila kitu kutoka kwao, sio watu wa zama zao peke yake, bali hadi vizazi vilivyo kuja baada yao, maendeleo makubwa ya kielimu yalishuhudiwa katika ulimwengu wa kiislamu.

Hakika Imamu huyu mtakatifu alikua kiongozi wa maisha ya maadili mema na kielimu.
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: