Sikukuu ya Ghadiir ambayo huadhimishwa mwezi kumi na nane Dhulhijjah, tukio la Ghadiir lilifanyika mwaka wa kumi hijiriyya, ni tukio ambalo Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipewa amri na Mwenyezi mungu ya kumtangaza Ali bun Abu Twalib (a.s) kuwa khalifa, wasii, Imamu na kiongozi baada yake. Nayo ni siku tukufu, hadithi zimetaja utukufu wa siku hiyo, tukio hilo ni la pili kwa utukufu katika uislamu baada ya tukio la kupewa utume na kushuka Quráni tukufu, katika riwaya iliyopokewa na Imamu Ali bun Mussa Ridhwa (a.s) kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake anasema: (Hakika siku ya Ghadiir ni mashuhuri zaidi mbinguni kushinga ardhini).
Kutoka kwa Imamu Jafari bun Abu Muhammad Swadiq (a.s) amesema: (..na jina lake mbinguni inaitwa siku ya ahadi iliyo ahidiwa na ardhini siku ya makubaliano na kundi shuhudiwa), kutoka kwa Imamu Ridhwa (a.s) anasema: (Wallahi lau watu wakijua utukufu wa siku hii kwa uhakika wangesalimiwa na malaika mara kumi kila siku).
Imepokewa kutoka kwa Imamu Jafari bun Muhammad Swadiq kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu zake (a.s) anasema: (Mtume (s.a.w.w) anasema: Ghadiir Khum ndio sikukuu bora katika umma wangu, ndio siku aliyoniamrisha Mwenyezi Mungu kumtawalisha ndugu yangu Ali bun Abu Twalib (a.s) kuongoza umma wangu baada yangu, nayo ni siku aliyokamilisha Dini na akakamilisha neema, na akaridhia kuwa uislamu ndio Dini…).
Katika siku hiyo Mtume (s.a.w.w) aliamrishwa na Mwenyezi Mungu mtukufu akusanye maelfu ya maswahaba wake katika sehemu ya katikati ya Makka na Madina iitwayo Ghadiir Khum, baada ya kumaliza ibada ya hijja, kuanzia hapo siku hii ikaanza kuitwa kwa jina la sehemu hiyo.
Mwenyezi Mungu mtukufu alikamilisha Dini na akatimiza neema yake kwa waumini kwa kumtawalisha kiongozi wa waumini Ali bun Abu Twalib (a.s), kuwa khalifa, wasii na Imamu baada ya Mtume (s.a.w.w) katika siku ya Ghadiir Khum, kwa hiyo siku ya Ghadiir ni siku tukufu mno, ni sikukuu kubwa ya Mwenyezi Mungu, kila mtume alisherehekea siku hiyo, kwa sababu ni siku ya kukamilishwa Dini na kutimizwa neema, kitu gani bora zaidi ya kukamilika Dini na kutimizwa neema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake, waumini wanatakiwa kushukuru na kuadhimisha neema waliyo pewa na Mwenyezi Mungu katika siku hii tukufu.
Abu Muayyad Muwafiq bun Ahmad Almakkiy Alkhawarizamiy aliyekufa mwaka wa 568 hijiriyya kwa sanadi ya Abu Saidi Khudriy anasema: Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alipoita watu kwa Ali (a.s) katika eneo la Ghadiir Khum, siku ya Alkhamisi, alimwita Ali akamshika mkono na kuupandisha juu hadi watu wakaona weupe wa kwapa ya Mtume (s.a.w.w), maswahaba hawakusambaa hadi iliposhuka aya hii.. (Leo nimewakamilishia Dini yenu na nimewatimizia neema yangu na nimekuridhieni Dini ya uislamu…), Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akasema: (Mwenyezi Mungu ni mkubwa kwa kukamilika Dini na kutimia neema na kuridhia ujumbe wanyu na uongozi wa Ali baada yangu).