Kitabu cha Arbabu Sira kimeandika kuwa mwezi kumi na mbili Muharam mwaka wa (61h) msafara wa mateka uliwasili Kufa, baada ya kuondoka Karbala siku ya mwezi kumi na moja, wakiwa na kumbukumbu zinazo umiza kwa kulala karibu na miili ya mashahidi, baada ya kuuwawa Imamu Hussein (a.s) na watu wa nyumbani kwake na wafuasi wake, watu wa Kufa wakafadhaika sana na wakatoka majiani, baadhi wao wakiwa hawajui mateka hao ni wakina nani na wengine wanajua na kulia kwa uchungu.
Msafara wa mateka ulielekea katika qasri la utawala, ukishindikizwa na kundi la watu wa Kufa wakiwa wanalia kwa kilicho wapata watu wa nyumba ya Mtume na kitendo cha kuvunja ahadi kwa mjukuu wa Mtume (s.a.w.w) na Imamu wa waislamu Hussein (a.s), leo familia yake wamekuwa mateka, na kichwa chake kinazungushwa katika mitaa ya Kufa kikiwa juu ya mkuki mrefu, wakati walimwita awe kiongozi wa waislamu.
Bibi Zainabu (a.s) aliwaangalia kwa hasira huku akiwa na uchungu mkubwa wa kufiwa kaka yake na familia yake, akatoa khutuba kali.
Kichwa cha Imamu Hussein (a.s) kikaingizwa katika qasri la utawala, na kuwekwa mbele ya ibun Ziyadi (laana iwe juu yake) akaanza kukipiga piga kwa finbo aliyokuwanayo mkononi kwake, huku akiwa na furaha, kisha wanawake, watoto na Ali bun Hussein (a.s) wakaingizwa, ibun Ziyadi akaanza kumuambia Zainabu (a.s) kwa dharau na kejeli, akasema: Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu ambae amekufedhehesheni, kakuuweni na kukadhibisha uzushi wenu. Bibi Zainabu akamjibu kwa kujiamini, akasema: (Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu ambae ametukirimu kwa Mtume wake Muhammad –s.a.w.w- na ametutakasa na uchafu, hakika mwenye fedheha ni mtu muovu na muongo wala sio sisi). Ibun Ziyadi akasema: Umeona Mwenyezi Mingu alivyo wafanya watu wa nyumbani kwako? Akasema: (Wale ni watu ambao Mwenyezi Mungu aliwaandikia shahada, na mtakutana wewe na wao mbele ya Mwenyezi Mungu na kuhojiana).
Ukafika wakati wa Imamu Sajjaad (a.s) akasimama mbele ya ibun Ziyadi, akauliza: wewe ni nani? Akamjibu: (Mimi ni Ali mtoto wa Hussein). Akasema: Mwenyezi Mungu hajamuuwa Ali bun Hussein? Akamjibu: (Nilikuwa na kaka anaitwa Ali ameuliwa na watu). Ibun Ziyadi akasema: Ameuliwa na Mwenyezi Mungu. Imamu (a.s) akamjibu: (Mwenyezi Mungu huchukua nafsi wakati wa kifo chake), Ibun Ziyadi akachukia kwa majibu ya Sajjaad (a.s), akamwita muuwaji akamuambia mkate shingo lake. Bibi Zainabu (a.s) akamkubatia mtoto wa kaka yake, na akasema: (Ewe ibun Ziyadi inatosha kumwaga damu zetu, wallahi sitamuachia ukimuuwa uniuwe pamoja nae), akaacha kumuua.
Ukatili wa ibun Ziyadi haukuishia hapo, siku ya pili aliendelea kuamrisha kichwa cha Imamu Hussein (a.s) kizungushwe katika mitaa ya Kufa, kuwatisha watu wa mji huo na kuvunja moyo wa upinzani dhidi yake.