Dondoo za kumbukumbu: Mwezi ishirini na tano Muharam ni siku ya kukumbuka kifo cha Imamu Zainul-Aabidina (a.s)

Maoni katika picha
Wapenzi na wafuasi wa maimamu wa Ahlulbait (a.s) katika siku kama ya leo mwezi ishirini na tano Muharam, wanakumbuka msiba mkubwa uliotokea katika nyumba ya Mtume na mashukio ya wahyi, msiba wa kuuwawa kishahidi Imamu Ali bun Hussein Sajjaad (a.s) katika mwaka wa (94h).

Kila ulipo ongezeka umri wa Imamu Zainul-Aabidina (a.s) aliendelea kudhofika, alikuwa mwingi wa kuabudu na kufanya twaa, alikuwa anafunga mchana na kusimama usiku, huku akikumbuka yaliyomtokea baba yake na watu wa nyumbani kwake katika ardhi ya Karbala, alikuwa kila anapo muangalia shangazi yake na dada zake anakumbuka namna walivyokuwa wanakimbia siku ya Ashura kutoka hema moja hadi lingine huku adui akisema: chomeni mahema ya madhalimu, anahuzunika sana hadi huzuni hizo zilisababisha kudhofika afya yake.

Imamu alikuwa anakubalika sana, watu walikuwa wanazungumzia elimu yake na ibada zake pamoja na subira yake, kila mtu alipenda kumuangalia na kumsikiliza, jambo hilo liliwaumiza sana bani Ummayya kwa ujumla na Walidi bun Abdulmalik akaweka uadui mkubwa.

Imepokewa kutoka kwa Zuhuriyyu kuwa Walidi bum Abdulmalik alisema: Sina raha madam Ali bun Hussein yupo duniani. Muovu huyo akakusudia kumuua pindi atakapo chukua utawala. Baada ya kupata utawala alimpa sumu kali mfanyakazi aitwae Yathriba na akamuamrisha amuwekee Imamu, mfanyakazi huyo akatekeleza akizo na kumuwekea sumu Imamu, baada ya kula sumu hiyo alisikia maumivu makali sana, akaugua kwa siku kadhaa, akawa anamshtakia Mwenyezi Mungu na kuomba maghrira, watu walimiminika kumuangalia (a.s), walimkuta muda wote anamsifu Mwenyezi Mungu kwa maneno mazuri na kumshukuru kwa kumruzuku kuuliwa kishahidi na kiumbe muovu.

Ugonjwa uliongezeka hali ikawa mbaya, sumu ikaenea mwili mzima, Imamu akawaambia wanafamilia yake kuwa atakwenda katika pepo ya Firdausi na akazimia mara tatu, alipo zinduka akasoma surat Fat-ha na surat Innaa fatahnaa kisha akasema (a.s): kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu ambae amesadikisha ahadi yake na ametupa pepo tunayo zunguka tutakavyo ni malipo bora kabisa kwa waabudio, roho yake tukufu ikatoka kama zinavyo toka roho za mitume na manabii, ikishindikizwa na malaika wa Mwenyezi Mungu.

Roho hiyo takatifu ilikwenda kwa Mola wake baada ya kuangaza dunia kwa elimu yake na ibada zake, na kujitenga na kila aina ya matamanio ya nafsi.

Imamu Abu Jafari Baaqir (a.s) akaandaa mwili wa baba yake, watu wakaona viungo vya sajda vinasugu kama vile sugu za magoti ya ngamia kutokana na wingi wa kusujudu kwake, na kwenye mabega wakaona sugu kubwa sawa na kwenye viungo vya sajda, wakamuuliza Imamu Baaqir (a.s) kuhusu sugu hizo, Imamu akasema: sugu za mabegani zinatokana na mfuko aliokuwa anabeba chakula na kwenda kugawa kwa mafakiri na watu wenye shida, baada ya kuoshwa, akavishwa sanda na kuswaliwa.

Jeneza lake lilishindikizwa na umati mkubwa sana wa watu ambao haukuwahi kushuhudiwa katika mji wa madina, wema kwa waovu wote walishiriki kwenda kumzika, huzuni kubwa ikaenea katika mji, vilio vikasikika kila mahala, kifo chake kiliwafanya wakose kheri nyingi, walikosa hali ya utulivu wa kiroho isiyokuwa na mfano, hali hiyo iliwapelekea watu wote wa madina kukusanyika kwenye msiba huo.

Jeneza likabebwa kwa takbira na tahmiid hadi kwenye makaburi ya Baqii Gharqad, wakamchimbia kaburi jirani na kaburi la Imamu Hassan bwana wa vijana wa peponi na mjikuu wa Mtume (s.a.w.w), Imamu Baaqir (a.s) akaingiza muili wa baba yake ndani ya kaburi, alizikwa pamoja na elimu, wema, taqwa na mazingira ya kiroho ya mitume na wachamungu.
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: