Vituo vya Ashura: Kifo cha kipenzi wa Hussein (a.s) kwenye kichwa cha baba yake

Maoni katika picha
Imepokewa na baadhi ya wanahistoria kuwa familia ya Hussein (a.s) na wajane wa nyumba ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) baada ya kuuwawa wanaume wao siku ya Twafu, walitekwa na kutembezwa mji baada ya mji, walikuwa wanawaficha watoto wadogo na mayatima kuuwawa kwa wazazi wao, alipolia mtoto alibembelezwa kwa upole, na walimuambia kuwa mzazi wake yuko safarini ipo siku atarudi, hiyo ndio njia waliyo tumia kupunguza machungu ya mayatima.

Imamu Hussein (a.s) alikuwa na binti mdogo aliye mpenda sana na yeye pia alimpenda sana, alikua anaitwa (Ruqayyah), alikua na umri wa miaka mitatu au minne, tangu siku ya kuuwawa kwake hakumuona, akawa mpweke kwa kumkosa baba yake, na alichukuliwa mateka hadi Sham, alikuwa anamlilia baba yake usiku na mchana, alikua anaambiwa kaenda safarini na kesho atarudi akiwa na vitu unavyo taka.

Siku moja akamuota baba yake usingizini, alipo amka alipiga kelele na akalia sana, kisha akasema: Nileteeni baba yangu burudisho wa macho yangu, mimi nimemuota kabla ya muda mfupi, kila walipo jaribu kumbembeleza alilia zaidi, watu wa nyumba ya Mtume (a.s) likawahuzunisha sana jambo hilo, wote wakaanza kulia, huzuni ikatanda vilio vikaenea.

Yazidi akaamka usingizini, akauliza: kuna nini? Akaambiwa kuwa mtoto mdogo wa Hussein amemuona baba yake usingizini na baada ya kuamka anamlilia.

Yazidi alipo sikia hivyo akasema: Mleteeni kichwa cha baba yake na mkiweke mbele yake ili amuone na anyamaze, wakaleta kichwa cha baba yake kikiwa kwenye sinia kimefunikwa kitambaa, wakamuwekea mbele yake, akauliza: kitu gani hiki? Mimi namtaka baba sio chakula, wakamuambia: Huyu ndio baba yako, kisha wakafunua kile kitambaa, akaona kile kichwa, akasema: hiki kichwa cha nani? Wakamuambua: hakika hicho ni kichwa cha baba yako, akakichukua kwenye sahani na kukikumbatia kifuani kwake huku anasema:

Ewe baba yangu nani amemwaga damu yako?

Ewe baba yangu nani amekata shingo lako?

Ewe baba yangu nani amenifanya kuwa yatima nikiwa na umri mdogo?

Ewe baba yangu nani nimtegemee baada yako?

Ewe baba yangu mimi yatima wa nani hadi nitakapo kuwa?

Ewe baba yangu nani atawaangalia wanawake wanyonge?

Ewe baba yangu nani atakaefuta machozi ya watu wanaolia?

Ewe baba yangu nani atawasaidia waliopotea na wageni?

Ewe baba yangu nani baada yako hakika tumepata hasara!.

Ewe baba yangu nani baada yako, ee ugeni wetu!. Ewe baba yangu laiti ningekuokoa.

Ewe baba yangu laiti ningekuwa kipofu kabla ya leo.

Ewe baba yangu laiti ningekufa kabla yaleo, nisingeona ndevu zako zikiwa zimelowa damu.

Kisha akaweka mdomo wake kwenye mdomo mtakatifu wa baba yake, akalia sana hadi akazimia, walipo muondoa akawa tayali ameaga dunia.
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: