Siku ya mwezi kumi na mbili Ramadhani lilitokea tukio muhimu katika historia ya kiislamu, katika siku hiyo mwaka wa kwanza hijiriyya Mtume (s.a.w.w) aliunga undugu kati yake na kiongozi wa waumini Ali (a.s) baada ya kuunga undugu baina ya Muhajirina na Answari.
Ahmadi bun Hambali na wengine wamesema kuwa: Mtume (s.a.w.w) aliunga undugu baina ya Muhajirina na Answari, na kumuacha Ali bila kumuunga undugu na mtu yeyote, akasema (a.s): Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu umeunga undugu baina ya maswahaba zako wote na umeniacha pekeyangu?
Akasema: Nimekuacha kwa ajili yangu, wewe ni ndugu yangu na mimi ni ndugu yako, ukiulizwa na yeyote sema: Mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu na ndugu wa Mtume wake, hakuna atakae sema hilo tofauti na wewe ispokua atakua muongo, naapa kwa aliyenipa Utume, wewe kwangu ni sawa na Haruna kwa Musa, ispokua hakuna Utume baada yangu, wewe ni ndugu yangu na mrithi wangu…
Kazi ya kwanza aliyofanya Mtume (s.a.w.w) baada ya kujenga msikiti ilikua ni kuunga undugu, ndio jambo kubwa lililo waunganisha Muhajirina na Answari, undugu wenye misingi ya Imani na mapenzi ya kweli ya kuokoana na kulindana, pamoja na kugawana sawa mali na vitu, hakika uhusiano uliimarika kwa kuunga undugu, aliwahi pia kuunga undugu baina ya Muhajirina alipokua Maka kabla ya kuhama, na kwa mara nyingine akaunga undugu kati ya Muhajirina na Answari baada ya kuhamia Madina.
Jambo la kuunga undugu alilofanya Mtume (s.a.w.w) lilikua tukio kubwa la siasa ya kiislamu inayo himizwa na Quráni tukufu, Mwenyezi Mungu anasema: (Hakika waumini ni ndugu).