Katika siku kama ya leo mwezi kumi na moja Dhulqaadah mwaka wa (148) hijiriyya iliangaza nuru katika mji wa Madina kwa kuzaliwa Imamu wa nane Ali bun Mussa Ridhwa (a.s).
Shangwe na furaha ikaingia katika nyumba ya Imamu Mussa bun Jafari (a.s) kwa kuzaliwa kwake, furaha ikaenea kwa watu wote wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w), Imamu Mussa Alkadhim alifurahi zaidi kwa kupata mtoto huyo mtukufu.
Imepokewa kutoka kwa Najma mama wa Imamu Ridhwa (a.s) anasema: Nilipo pata ujauzito wa mwanangu Ali sikuona udhia wowote, nilikua nikilala nasikia tasbihi, tahliil na tamjiid tumboni mwangu, jambo hilo lilinifadhaisha, nikiamka sisikii kitu, nilipo jifungua, alitoka na kuweka mikono yake ardhini, akiwa ameinua kichwa chake juu huku midomo yake inatikisika, kamavile anaongea, akaingia baba yake Mussa bun Jafari (a.s) akaniambia: Hongera ewe Najma Mwenyezi Mungu amekukirimu, nikampa akiwa kwenye kitambaa cheupe, akamuadhinia katika sikio la kulia na kukim katika sikio la kushoto kisha akachukua maji ya Furaat na kumweka mdomoni ahafu akamrudisha kwangu na kusema: mchukue hakika huyu ni kielelezo cha Mwenyezi Mungu katika Ardhi.
Imamu Ridhwa (a.s) alikulia katika nyumba tukufu zaidi hapa duniani, nyumba ya Uimamu na mashukio ya wahyi, nyumba aliyo idhinisha Mwenyezi Mungu litajwe na kutukuzwa jina lake, alipata malezi bora kabisa ya kiislamu, alimuheshimu mkubwa na kumhurumia mdogo, alikuwa na adamu kubwa na tabia njema, muda wote alisikika akisoma kitabu cha Mwenyezi Mungu na kuhimiza kufanya wema na kila kitu kinacho mkurubisha mwanaadamu kwa Mola wake.
Hakika Imamu Ridhwa (a.s) alipambika na kila aina ya tabia njema, hakuna jambo zuru analo sifika nalo mwanaadamu ispokuwa alikuwa nalo, Mwenyezi Mungu mtukufu alimtunuku ukamilifu kama alivyo watunuku wazazi wake watakatifu, na akamfanya kuwa kiongozi katika umma wa babu yake.