Mwezi ishirini Safar kwa mujibu wa baadhi ya riwaya na vitabu vya Historia, msafara wa mateka wa Hussein (a.s) uliwasiri Karbala mwaka wa 61h, ikiwa ni siku ya arubaini tangu yalipotokea mauaji ya kinyama yaliyo pelekea kuuawa Imamu Hussein (a.s) na watu wa nyumbani kwake na wafuasi wake watukufu.
Riwaya zinasema kuwa wakati msafara wa mateka unatoka Sham kurudi Madina, ulifika njia panda ya kwenda Iraq na Hijazi, wakamuambia muongozaji wa njia, tupitishe Karbala, wakafika Karbala siku ya mwezi ishirini Safar -siku ya Arubaini-, wakazuru kaburi la Imamu Hussein (a.s) na watu wa nyumbani kwake na wafuasi wake, wakafanya vikao vya kuomboleza na kukaa hapo siku kadhaa.
Kutoka kwa Atwiyya Aufi anasema: Nilitoka na Jaabir bun Abdillahi Answari (r.a) kwenda kuzuru kaburi la Hussein (a.s), tulipofika Karbala Jaabir akaenda kwenye mto wa Furaat, akaoga kisha akajifunga shuka na nyingine akajifunika, halafu akajipaka marashi, kisha akamtaja Mwenyezi Mungu mtukufu, alipokaribia kwenye kaburi akasema: Nigusishe. Nikamgusisha, akaanguka juu ya kaburi na kuzimia, nikamwagia maji. Alipo zinduka akasema: Ewe Hussein (mara tatu). Kisha akasema: Mpenzi hamuachi mpenzi wake, hauwezi kujibu, wamekukata shingo lako na wakatenganisha baina ya mwili na kichwa chako. Nashuhudia wewe ni mtoto wa Mtume wa mwisho, mtoto wa bwana wa waumini, mtoto wa mchamungu na nguzo ya uongofu, wewe ni wa tano katika watu wa shuka (As-habul-kisaa), mtoto wa Fatuma mbora wa wanawake. Kwa nini usiwe hivyo wakati umelishwa na mkono wa mbora wa mitume, umelelewa kwenye miguu ya wachamungu, umenyonya maziwa ya Imani, ulikua mzuri ukiwa hai na bado ni mzuri baada ya kufa kwako, nyoyo za waumini hazina furaha kukukosa, wala hazikupata shida wakati wa uhai wako, amani ya Mwenyezi Mungu na radhi zake ziwe juu yako, nashuhudia kuwa umepita njia aliyopita ndugu yako Yahaya bun Zakariyya.
Kisha akazunguka kaburi na kuelekea makaburi mengine halafu akasema: Amani iwe juu yenu enyi roho mliokufa kwa ajili ya Hussein (a.s), nashuhudia kuwa mlisimamisha swala na mkatoa zaka, mliamrisha mema na kukataza mabaya, mkapigana jihadi na kumuabudu Mwenyezi Mungu hadi mlipofikwa na kifo.
Naapa kwa aliyemtuma Muhammad kuwa Mtume, tumeshirikiana nanyi katika mliyoyapata. Atwiyya akasema: vipi na hatukuwa pomoja nao jangwani, wala hatukupanda nao mlima, wala kupigwa panga?!. Na wao wametenganishwa miili na vichwa vyao, na watoto wao wamebaki mayatima, wake zao wamebaki wajane?!.
Akasema: Ewe Atwiyya, nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) anasema: (Atakaependa watu atafufuliwa pamoja nao, na atakaependa kazi ya watu atashirikishwa kwenye kazi yao). Naapa kwa aliyemtuma Muhammad kwa haki hakika nia yangu ikopamoja na hussein (a.s) na wafuasi wake.
Atwiyya akasema: Wakati tukiongea hayo mara niliona weusi umechomoza upande wa Sham. Nikasema ewe Jaabir, kuna msafara unakuja kutoka upande wa Sham. Jaabir akasema: nenda kaangalie halafu uje uniambie, kama wakiwa ni watu wa Omari bun Saadi rudi haraka tutafute sehemu ya kujificha, akiwa ni Zainul-Aabidina (a.s) utakua huru kwa haki ya Allah mtukufu.
Akaenda, baada ya muda mfupi akarudi huku anasema: Ewe Jaabir, simama upokee haram ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w). Huyu ni Zainul-Aabidina (a.s) amekuja na shangazi yake na dada zake.
Jaabir akasimama na kutembea bila viatu huku akiwa kichwa wazi, hadi alipofika kwa Zainul-Aabidina (a.s), Imamu (a.s) akasema: Wewe ni Jaabir? Akasema: Ndio ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akasema: Ewe Jaabir, Wallahi hapa ndipo walipouawa watu wetu, walichinjwa watoto wetu na kutekwa wanawake wetu, na kuchomwa hema zetu.
Tukio hilo ndio kikao cha kwanza cha kuomboleza Arubaini ya Imamu Hussein (a.s)..