Kumbukumbu ya kuzaliwa Kauthara mtoto wa Mtume Fatuma Zaharaa (a.s)

Maoni katika picha
Siku kama ya leo mwezi (20) Jamadal-Aakhar alizaliwa mbora wa wanawake Fatuma Zaharaa (a.s), pande la damu la Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika mwaka wa tano wa utume, wakati huo Mtume alikua na umri wa miaka arubaini na tano, hivyo aliishi Makka miaka nane na Madina miaka kumi.

Shekhe Swaduqu amepokea kwa sanadi nzuri kutoka kwa Mufadhil bun Omari anasema: Nilimuuliza Abu Abdillahi (a.s), yalikua vipi mazazi ya Fatuma (a.s)? akasema: Hakika Khadija alipoolewa na Mtume (s.a.w.w) wanawake wa Maka walimtenga, wakawa hawaingii nyumbani kwake wala hawamsalimii, bibi Khadija akawa mpweke, alipopata ujauzito wa Fatuma, bibi Fatuma akawa anaongea nae akiwa tumboni mwake na kumtaka avumilie, na akawa anaficha jambo hilo kwa Mtume (s.a.w.w).

Siku moja Mtume (s.a.w.w) alipoingia ndani akamsikia Khadija anaongea na Fatuma, akamuuliza: Ewe Khadija unaongea na nani? Akasema: Mtoto aliyetumboni mwangu ananiongelesha na kuniliwaza, akasema: Ewe Khadija Jibrilu ameniambia mtoto huyo ni mwanamke na hakika ni mtakasifu, na Mwenyezi Mungu atajaalia kizazi changu kutokana na yeye, na atajaalia Maimamu kutokana na kizazi chake watakua makhalifa katika ardhi baada ya kuisha wahayi.

Khadija aliendelea kuwa katika hali hiyo hadi alipokaribia kujifungua, akawaita wanawake wa kikuraishi na bani Hashim waje kumsaidia wakati wa kujifungua, wakamjibu kuwa wewe umetuasi na ukaolewa na Muhammad yatima wa Abu Twalib fakiri asiyekuwa na mali, hatuji wala hatukusaidii chochote.

Bi Khadija (a.s) akahuzunika kwa majibu hayo, akiwa katika hali hiyo ghafla waliingia wanawake wanne warefu kama wanawake wa bani Hashim, akashtuka. Mmoja wao akamuambia usihuzunike ewe Khadija, Mola wako ametutuma kwako, sisi ni dada zako, mimi ni Sara na huyu ni Asia binti Muzahim naye ni Rafiki yako peponi, na huyu ni Maryam binti Imraan na huyu ni Kulthum dada wa Mussa bun Imraan, Mwenyezi Mungu ametutuma kwako kuja kukusaidia wakati wa kujifungua, mmoja akakaa kuliani kwake na mwingine kushotoni kwake wa tatu akakaa mbele yake na wa nne akakaa nyuma yake, akazaliwa Fatuma akiwa msafi, alipo toka nuru iliangaza hadi ndani ya nyumba za watu wa Maka, na ikaangaza dunia nzima mashariki na magharibi, wakaingia mahuruan kumi, kila mmoja akiwa ameshika chombo (beseni) na birika la maji ya mto wa Kauthar kutoka peponi.

Wakapokewa na mwanamke aliyekua amekaa mbele yake, akamuogesha kwa maji wa Kauthar na akachukua vitambaa viwili vyeupe kushinda maziwa na vinaharufu nzuri kushinda miski, akamfunika kisha akamsemesha, Fatuma (a.s) akamuitikia kwa kutamka shahada mbili, alisema: Nashuhudia kuwa hakuna Mungu ispokua Allah na hakika baba yangu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mbora wa Mitume na mume wangu ni bwana wa mawasii na watoto wangu ni mabwana wa wajukuu.

Kisha akawasalimia na akataja jina la mmoja baada ya mwingine, wakaanza kucheka, Huruain na viumbe wa mbinguni wakapeana habari ya kuzaliwa kwa Fatuma (a.s) ikatokea nuru kubwa mbinguni ambayo ilikua haijawahi kushuhudiwa na Malaika kabla ya hapo. Wale wanawake wakasema: Mchukue ewe Khadija ni msafi na mtakasifu, amebarikiwa yeye na kizazi chake, bi Khadija akamchukua akiwa amejaa furaha na kumuweka kifuani na akaanza mumnyonyesha, bibi Fatuma (a.s) alikua anakua kwa siku sawa na makuzi ya mtoto mwingine kwa mwezi, na kwa mwezi sawa na makuzi ya mtoto mwingine kwa mwaka.
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: