Leo siku ya Jumamosi mwezi kumi na tano Shabani, ulimwengu wa kiislamu unaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa muokozi wa binaadamu msubiriwa Imamu Mahadi (a.f).
Naye ni Imamu wa kumi na mbili katika Maimamu wa Ahlulbait (a.s) walio bashiriwa na Mtume (s.a.w.w), pale aliposema: (Baada yangu kunamakhalifa kumi na mbili wote wanatokana na makuraishi), nao ni katika kizazi cha bibi Fatuma Zaharaa (a.s) na katika wajukuu wa Imamu Hussein Shahidi (a.s).
Vitabu vya historia na riwaya vimeeleza mazazi ya Imamu Muhammad msubiriwa (a.f) kuwa, ilikua ni kawaida ya bibi Hakima (mtoto wa Imamu Aljawaad na shangazi wa Imamu Hassan Askariy a.s), kila anapomtembelea mtoto wa kaka yake anamuomba Mwenyezi Mungu amruzuku mtoto wa kiume, anasema: alienda kwake siku moja, akaomba dua kama kawaida yake, akasema: ewe shangazi hakika maombi yako kwangu yamekubaliwa, Mwenyezi Mungu ataniruzuku mtoto usiku huu, leo lala kwetu hakika atazaliwa mtoto mtukufu, bi Hakima akauliza, nani atajifungua ewe kiongozi wangu, sioni athari ya ujauzito kwa Narjisi. Akasema: huyo huyo Narjisi hakuna mwingine.
Akasema: Nikamkumbatia Narjisi nikamuangalia mgongoni na tumboni sikuona athari ya ujauzito, nikaenda kumuambia kuwa nimemkagua hana ujauzito, akatabasamu kisha akasema: ukifika wakati wa Alfajiri utaona athari ya ujauzito, kwa sababu mfano wake ni sawa na mama wa Nabii Mussa, athari ya ujauzito wake haikuonekana, hakuna aliyejua kama anaujauzito hadi wakati wa kujifungua, kwa sababu Firauna alikua anapasua matumbo ya wakinamama wajawazito kwa ajili ya kumtafuta Mussa (a.s) na huyu ni mfano wa Nabii Mussa (a.s) atamaliza utawala wa Firauni.
Hakima akasema: Nikaendelea kumuangalia hadi wakati wa Alfajiri huku akiwa amelala mbele yangu, ulipofika wakati wa Alfajiri akashtuka, nikamkumbatia, Imamu akaniambia msomee (Innaa anzalnaahu fii lailatulqadri..), nikaanza kumsomea kama nilivyo elekezwa, akaniitikia mtoto aliye tumboni, akawa anasoma kama ninavyo soma.
Bi Hakima anasema: Nikashtuka, Imamu Askariy akasema: Usishangae amri ya Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu humzungumzisha atamkae akiwa mdogo, na kumfanya kuwa hoja kwa waja wake anapokua mkubwa, kabla hajamaliza kuongea bibi Narjisi akatoweka machoni kwangu, sikumuona kanakwamba imewekwa pazia baina yetu, nikaenda upande alipo Imamu Askariy (a.s), akaniambia: Rudi ewe shangazi yangu utamuona palepale.
Akasema: Nikarudi baada ya muda mfupi ikaondolewa pazia baina yetu, nikamuona akiwa anatoka nuru, mara nikamuona mtoto akiwa kasujudu, kisha akainua mikono yake na kusema: (Ashhadu an laa ilaaha Illa Llahu wahdahu laa sharikalahu, wa anna jadii Rasulullah (s.a.w.w) wa anna abii Amirulmu-uminina…) kisha akataja Imamu mmoja baada ya mwingine hadi akafika kwake, akasema (a.s): Ewe Mwenyezi Mungu, nitimizie ahadi na unikamilishie amri, unipe nguvu ya kuijaza dunia haki na uadilifu…