Maahadi ya Qur’ani tukufu chini ya Majmaa ya Qur’ani katika Atabatu Abbasiyya na matawi yake yaliyopo mikoani, asubuhi ya siku ya Jumatano zimeanza semina za majira ya joto zikiwa na wanafunzi zaidi ya (25,000).
Mkuu wa Maahadi Shekhe Jawadi Nasrawi ameuambia mtandao wa Alkafeel kuwa: “Mradi huu umerudi tena baata ya kusimama kwa miaka miwili kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya Korona, ambapo ililazimika semina hizi kufanywa kwa njia ya mtandao”.
Akaongeza kuwa: “Masomo yataendeshwa ndani ya haram ya Abulfadhil Abbasi (a.s), kwenye shule za Al-Ameed, ndani ya Misikiti, Husseiniyya, na maeneo mengine katika mikoa ya Bagdad, Baabil, Diwaniyya, Muthanna, wilaya na Hindiyya, chini ya usimamizi wa wabobezi wa masomo ya Qur’ani”.
Akabainisha kuwa: “Katika semina hizi watafundishwa (Kuhifadhi Qur’ani, Fiqhi, Aqida, Akhlaq, Historia ya Ahlulbait a.s), pamoja na ratiba ya michezo na mapumziko, program yote inalenga kujenga utamaduni wa kufanyia kazi vizito viwili katika nafsi za vijana”.
Kumbuka kuwa semina hizi ni sehemu ya harakazi ya Maahadi ya Qur’ani, ambayo hufanywa kila mwaka kwa makundi tofauti ya jamii, hususan kwa wanafunzi wa shule tofauti, ambapo hutumia muda wa likizo za majira ya joto kufanyia kazi kauli ya Mtume (s.a.w.w) isemayo: (Wafundisheni watoto wenu mambo matatu: kumpenda Mtume wenu, kuwapenda watu wa nyumba yake na kusoma Qur’ani), sambamba na kufuata maelekezo ya Atabatu Abbasiyya tukufu katika swala la Qur’ani.