Historia zinasema kuwa Ubaidullahi bun Ziyadi -Gavana wa Kufa- alikua anatuma askari wake wa aina mbalimbali katika ardhi ya Karbala, miongoni mwa watu aliowapa jukumu la kupambana na Imamu Hussein (a.s) ni Omari bun Saadi na akamuahidi kama akifanikiwa kumuua Hussein (a.s) atampa ugavana katika mji wa Rai.
Omari bun Saadi akachagua Maisha ya kifalme hapa Duniani, akaongoza jeshi la wapiganaji elfu nne, wakaenda kuweka kambi karibu na hema la Imamu Hussein (a.s), waliwasiri hapo mwezi tatu Muharam mwaka 61h.
Kabla Omari bun Saadi hajaingia vitani na Imamu Hussein (a.s) walikutana na wakaongea, akamuandikia Ibun Ziyadi na kumuambia kuwa amefanya mazungumzo na Imamu, yuko tayali aruhusiwe kurudi alikotoka na kuepusha umwagaji wa damu unaotarajiwa kutokea katika ardhi ya Iraq.
Barua ya Omari bun Saadi ikawasiri kwa Ubaidullahi bun Ziyadi, naye akamuandikia majibu na akampa Shimri bun Dhijaushen apeleke, tunaandika machache yaliyopo katika barua hiyo.
Mimi sikukutuma kwa Hussein ukawe ngao yake, wala kuongea nae au kumpa amani, wala kumuombea msamaha, sikia, kama Hussein na wenzake wakitii utawala wangu walete kwangu salama, wakikataa wauwe na usulubu maiti zao, hakika wao wanastahiki kufanywa hivyo, akiuawa Hussein amuru farasi wakanyage kanyage kifua chake na mgongo wake hakika yeye ni dhalimu, kama huwezi kutekeleza hayo, acha jeshi letu na Shimri bun Dhijaushen ataongoza jeshi, tumesha mpa maagizo yetu, mwisho.
Omari bun Saadi akapokea barua, na akaisoma, akaanza kupambana na nafsi yake baina ya kupambana na Hussein (a.s) na kumuua, jambo litakalo mpa uongozi na Maisha ya kifalme, Pamoja na heshima kubwa mbele ya mabosi wake, na baina ya dhambi kubwa za kufanya unyama huo, nafsi yake ikachagua ufalme na mali, akaamua kuongoza vita na kumwaga damu takatifu chini ya usaidizi wa Shimri bun Dhijaushen.