Ofisi ya Muheshimiwa Marjaa-Dini mkuu Sayyid Ali Husseini Sistani, imetoa salamu za rambirambi kufuatia kuuawa kishahidi kwa Allamah Hujjatul-islami wal-muslimina Sayyid Hassan Nasrullah.
Ifuatayo ni nakala ya tamko:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu.
(Wapo watu miongoni mwa waumini waliotimiza ahadi waliyoahidiana na Mwenyezi Mungu, baadi yao wamekwishamaliza nadhiri zao na wapo miongoni mwao wamaongojea, wala hawakubadilisha (ahadi yao) hata kidogo).
Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kishahidi kwa Allamah Hujjatul-islami wal-muslimina Sayyid Hassan Nasrullah na wapiganaji wa Lebanon tukufu na makumi ya wananchi waliouawa katika shambulizi lililofanywa na jeshi la maadui la Izrael pembezoni mwa jiji la Bairuti.
Hakika shahidi alikuwa kiongozi bora, ni wachache watu kama yeye katika zama hizi, amepambana kwa namna ya pekee na walowezi wa Izrael katika kukomboa ardhi ya Lebanon, alisaidia raia wa Iraq kwa hali na mali katika kukomboa miji iliyotekwa na magaidi wa Daeshi, kama alivyojitolea katika kusaidia wananchi wa Palestina hadi kupelekea kuuawa kwake.
Tunatoa salamu za rambirambi kwa raia wa Lebanon na wananchi wadhulumiwa wote kufuatia msiba huu na hasara kubwa tuliyopata, tunamuomba Mwenyezi Mungu amuweke mahala pema peponi na amkutanishe na wapenzi wake Mtume Muhammad na kizazi chake kitakatifu, awape subira na utulivu familia yake na wafiwa wote kwa ujumla. Hakika sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.
(24 Rabiul-Awwal 1446h) sawa na (28/9/2024m)
Ofisi ya Sayyid Sistani – Najafu Ashrafu.