Siku ya tano katika mwezi wa Jamadil Ula alizaliwa bibi Zainabu katika nyumba takasifu na mzazi mtakasifu (maasuma) ambaye ni bibi wa wanawake wa duniani Fatuma Zaharaa (a.s) siri ya kiungu, ambaye alitokana na mtakasifu mbora wa viumbe wote mtume mtukufu Muhammad (s.a.w.w), na baba yake ni Amirulmu-uminina (s.a) na ndugu zake ni imamu Hassan Mujtaba na imamu Hussein Shahidi wa Karbala (a.s), akafumbua macho yake ndani ya nyumba ambayo tunaweza sema Jibrilu alikua ni mtumishi wao kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Pindi bibi Fatuma alipo jifungua alimpeleka mtoto kwa Amirulmu-uminina (a.s) akamuambia: mpe jina huyu mtoto, imamu akamjibu kwa unyenyekevu na adabu kubwa, siwezi kumtangulia mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), naye mtume alipo pata habari ya kujifungua kwa binti yake, alienda haraka katika nyumba yao, alipo fika imamu akamuomba ampe jina mtoto, mtume akajibu kua: siwezi kumtangulia Mwenyezi Mungu, ndipo mjumbe wa mbunguni (Jibrilu a.s) akaja kwa mtume na akamuambia kua: (Huyu mtoto mpe jina la –ZAINABU- Mwenyezi Mungu amemchagulia jina hili) kisha Jibrilu akamuambia mtume matatizo mazito yatakayo mkuta mjukuu wake, mabalaa na misiba mizito, mtume akamchukua mjukuu wake kwa uso wa huzuni huku machozi yanamtoka, akamuweka kifuani kwake na akawa anambusu, bibi Fatuma alishangaa kuona baba yake analia, akamuuliza: (Kitu gani kinakuliza ewe baba yangu? Mwenyezi Mungu hajapata kuyaliza macho yako?!!), mtume akamjibu kwa sauti ya chini iliyo jaa huzuni: (Ewe Fatuma tambua hakika binti huyu baada yangu na baada yako atapatwa na misiba na majonzi…) mtume pamoja na watu wa nyumbani kwake wakaendelea kulia.
Hakika mtume (s.a.w.w) alitambua hali ngumu itakayo mkuta mjukuu wake, matatizo ambayo majabali yanaweza kulainika, na kwamba atapata mitihani ambayo hajawahi kuipata bibi yeyote katika watoto wa Hawa, ni jambo la kawaida kua; pande lake la damu (bibi Fatuma) na mlango wake wa elimu (imamu Ali) walishirikiana na mtume (s.a.w.w) katika huzuni, halafu akaja Salmani Muhammadiy (Farsi) mfuasi mukhlisu (wa kweli) wa familia ya mtume (s.a.w.w) kumpongeza imamu Ali (a.s) kwa kupata mtoto mtukufu, akamkuta ni mwenye huzuni, huku anaelezea misiba itakayo mkuta mtoto wake, Salmani naye akashiriki katika machungu na huzuni zao.
Kuhusu jina lake (Zainabu) kuna kauli mbili:
Kauli ya kwanza: ni neno lililo pambika na maneno mawili (Zain) pambo na (Abu) baba (Zainabu=pambo la baba) hayo ni kwa mujibu wa Fairuzi Aabaadi katika kamusi ya Muhiitu.
Kauli ya pili: Zainabu ni neno moja na sio mawili, nalo ni jina la mti au uwa –kama ilivyo andikwa katika lisaanu arabu- Zainabu ni mti wenye muonekano mzuri na harufu nzuri pia huitwa wanawake jina hilo, na katika kitabu cha “Ausi” Zainabu ni mmea wa majani wenye maua mazuri ya rangi nyeupe yenye harufu nzuri.
Majina yake ya kunia anaitwa: Ummu Kulthum na Ummu Hassan, pia bibi Zainabu anaitwa Aqilah na waandishi wengi pamoja na makhatibu, huu ni wasifu wa bibi zainabu na sio jina lake, wasifu wa Aqilah una maana nyingi, miongoni mwake ni: mwanamke mkarimu, mwenye heshima na thamani kubwa. Amekua mashuhuri zaidi kwa kunia ya (Ummu Maswaaib) ni haki yake kuwa mashuhuri kwa kunia hii, hakika alishuhudia msiba wa babu yake mtume mtukufu (s.a.w.w) na wa mama yake shahidi madhlumu bibi wa wanawake wa duniani (a.s) na msiba wa kifo cha baba yake Haidari Alkarari (a.s) na mtihani wa kupewa sumu kwa kaka yake Hassan Mujtaba (a.s) na msiba mkubwa wa kaka yake Bwana wa Mashahidi (a.s) alio ushuhudia kuanzia mwanzo hadi mwisho, pamoja na kuuawa kishahidi kwa watoto wake Auni na Muhammad mbele yake na akachukuliwa mateka na kuendelea kutembea hadi Kufa kisha kutoka katika mji wa Kufa hadi Sham.
Miongoni mwa kilele cha utukufu wake na ukamilifu wa tabia zake ni kuipa nyongo dunia , alifata nyao za baba yake aliye ipa talaka tatu dunia zisizo kua na rejea, hali kadhalika aliiga tabia za mama yake bibi wa wanawake wa duniani Zaharaa (a.s) imepokewa na wanahistoria kua; alikua hamiliki ndani ya nyumba yake isipokua mkeka ulio tengenezwa kwa majani ya tende na ngozi ya mbuzi, alikua anavaa nguo iliyo tengenezwa kutokana na manyoya ya ngamia na alikua anasaga ngano kwa mikono yake, na mengineo mengi miongoni mwa sifa za zuhudi na kuipa nyongo dunia, miongoni mwa zuhudi zake kama ilivyo pokewa na imamu Zainul Aabideen (a.s), alikua haweki ndani ya nyumba yake kitu cha kutumia kesho, hakika aliitaliki dunia na kuipa nyongo kwa kufatana na kaka yake baba wa watu huru (Abul-ahraar) (a.s) huku akifahamu wazi kua atauliwa katika aridhi ya Karbala kama alivyo ambiwa na baba yake, akajitolea kusimama pamoja na kaka yake kwa ajili ya kunusuru uislamu na kutetea haki na utukufu, huku akifahamu wazi masaibu yatakayo msibu ya kuuliwa wa ndugu na watoto wa ndugu zake kisha yeye kuchukuliwa mateka, alijitolea yote hayo kwa ajili ya kuitumikia dini ya Mwenyezi Mungu mtukufu.
Bibi Zaibabu (a.s) ana nafasi kubwa sana katika tukio la Karbala na alikua na jukumu kubwa katika hali zote, alikua anafatilia hali ya kaka yake Hussein (a.s) kila wakati na kumuuliza katika kila tukio, ndiye aliye simamia familia na watoto, alisimama imara katika mazingira magumu, alikua anamuuguza Zainul Aabideen (a.s) na kumhami katika maeneo mengi, alikua akimliwaza Fatumat Sughra, kwa kua karibu naye na alichukua nguo za shangazi yake pindi aliposema mtu kutoka Sham kumuambia Zaidi: Nipeni mimi huyu mateka, hakika bibi Zainabu alikua ni nguzo imara.