Kipindi cha machungu baada ya shahada ya bibi Fatuma Zaharaa (a.s) na kuzikwa kwake..

Maoni katika picha
Ziliongezeka sauti za vilio katika nyumba ya Ali (a.s) na mji wote wa Madina ulijaa vilio wanaume kwa wanawake, watu walipatwa na mshituko sawa na siku aliyo fariki mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), wanawake wa banii Hashim wakakusanyika katika nyumba ya bibi Fatuma (a.s) wakawa wanalia humo, watu wakaenda kwa Ali (a.s) wakamkuta amekaa na watoto wake Hassan na Hussein wakiwa wanalia, Umu-kulthum akatoka huku akisema: Ewe baba yake ewe mtume wa Mwenyezi Mungu! Sasa hivi kweli tumekukosa hatuta kutana tena.

Watu wakakusanyika kwa wingi wakiwa wanalia, huku wanasubiri kutolewa jeneza walisalie, akatoka Abuu-dhari akasema: ondokeni hakika yameahirishwa maziko ya mtoto wa mtume hadi kesho.

Watu wakaondoka wakiwa wanadhani maziko yatafanyika asubuhi ya siku inayo fuata (Imepokewa kua alifariki baada ya Alasiri au mwanzoni mwa usiku).

Imamu Ali (a.s) pamoja na Asmaa walimuosha na wakamvisha sanda katika usiku ule, kisha imam akaita: (Ewe Hassan.. Ewe Hussein.. Ewe Zainabu na Umu-kulthum.. njooni mtoe zawadi kwa mama yenu leo mnaachana mtakutana peponi), baada ya muda Amirul-muuminina (a.s) aliwaambia waondoke. Kisha Ali (a.s) akaswalia jeneza, akainua mikono juu na akasema: (Ewe Mwenyezi Mungu huyu ni binti wa mtume wako Fatuma, umemtoa katika giza na kumpeleka katika nuru, muangazie maili kwa maili).

Usiku ulipo ingia sauti zikatulia watu wakalala, alitoka imamu Ali (a.s) na Abbasi, Fadhil bun Abbasi na Raabii wakiwa wameubeba muili mtukufu, wakasindikizwa na Hassan, Hussein, Aqeel, Salmaan, Abuu-dhari, Mikdadi, Buraida na Ammaar. Walipo fika kaburini, imamu Ali (a.s) akatelemka ndani ya kaburi na kuupokea muili mtakasifu na kuulaza katika mwana ndani huku akisema: (Ewe aridhi ninakukabidhi huyu binti wa mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu, Bismilahi wa bilahi wa alaa milati rasuli llaahi Muhammad bun Abdillahi (s.a.w.w), nakukabidhi ewe Swidiqa kwa yule ambaye ni bora kwako kuliko mimi, nimekuridhia kwa yale aliyo kuridhia Mwenyezi Mungu mtukufu) kisha akasoma aya isemayo: (Kutokana (na udongo) tumekuumbeni na katika (udongo) tutakurudisheni na kutoka katika (udongo) tutakutoeni kwa mara nyingine) kisha akatoka ndani ya kaburi, halafu watu walio kua pembezoni yake wakaanza kufukia kaburi tukufu walipo maliza Imamu Ali (a.s) akalisawazisha ili lisijulikane, halijulikani lilikua wapi na halitajulikana hadi siku ya kiama.

Sio ajabu wanahistoria kutofautiana kuhusu siku ya kufariki kwake na kiwango cha umri wake, kama walivyo tofautiana kuhusu tarehe ya kuzaliwa kwake kua ilikua baada ya utume au kabla ya utume, pia wametofautiana kuhusu siku alizo ishi baada ya kufariki kwa baba yake (s.a.w.w), hali kadhalika wametofautiana kuhusu sehemu aliyo zikwa, naye ni pande la damu ya mtume (s.a.w.w), baadhi ya wanahistoria wanasema alizikwa katika nyumba yake, na wengine wanasema alizikwa katika makaburi ya Baqee huku wengine wakisema alizikwa katika sehemu ya Raudha takasifu wakitegemea hadithi ya mtume (s.a.w.w) isemayo: (katikati ya minbari yangu na kaburi langu ni sehemu miongoni mwa sehemu za peponi), Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye ukweli. Yote haya ni dalili za wazi kuhusu kudhulumiwa kwake na matatizo aliyo kutana nayo katika maisha yake.
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: