Mwenyezi Mungu ayakuze malipo yako ewe Mtume kwa kufiwa na mama wa waumini bibi Khadija (a.s)..

Maoni katika picha
Katika siku kama ya leo tarehe kumi Ramadhani mwaka wa kumi wa utume, yaani; miaka mitatu kabla ya Mtume kuhama Maka na kwenda Madina, alifariki mama wa waumini bibi Khadija bint Khuwailid (a.s) ambaye alikua mke wa Kwanza wa mtukufu Mtume (s.a.w.w), na hakuwahi kuoa mke mwingine hadi alipo fariki.

Tukio la kufariki kwa bibi Khadija (a.s) lilikua na athari kubwa kwa Mtume (s.a.w.w), kwa sababu hakua ni mwanamke tu; bali alikua mwanamke wa mfano kwa ukamilifu, imani na kujitolea, alionyesha upeno wa hali ya juu na alijitolea kila kitu chake kwa ajili ya maisha ya Mtume (s.a.w.w).

Alijitolea mali, heshima na utukufu wake, bali alijitolea hadi nafsi na roho yake kwa ajili ya kumfurahisha mbora wa binadamu na mtukufu wa mitume ili amridhishe Mlezi wa viumbe wote na apate utukufu wa duniani na akhera, kifo chake kilimuumiza sana Mtume (s.a.w.w) na alihuzunika mno, hilo lilionekana wazi kwa Mtume (s.a.w.w), ukizingatia kua kifo chake kilitokea baada ya kufariki kwa Ammi yake Abutwalib (a.s), kutokana na ukubwa wa huzuni yake kwao Mtume (s.a.w.w) aliuita mwaka huo kua “mwaka wa huzuni” kwani misiba hiyo ilikua na athari kubwa sana kwa Mtume (s.a.w.w) na ilimuumiza mno.

Baada ya kufariki bibi Khadija (a.s) Mtume (s.a.w.w) alimuandaa akamuosha na kumpamba, alipotaka kumvisha sanda alikuja Jibrilu (a.s) akamuambia: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika Allah anakutumia salam na anasema kua: Ewe Muhammadi sanda ya Khadija ni jukumu letu, hakika yeye alitoa mali zake kwa ajili yetu”. Jibrilu akaja na sanda na akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hii sanda ya Khadija, nayo ni miongoni mwa sanda za peponi amepewa na Mwenyezi Mungu”.

Mtume (s.a.w.w) akamvisha kwanza sanda yake, kisha akamvisha sanda aliloletewa na Jibrilu, akawa kavishwa sanda mbili: Moja kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) na nyingine kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), akamzika katika makaburi ya Hajuun ndani ya mji mtukufu wa Maka, Mtume (s.a.w.w) akaingia ndani ya kaburi lake kumzika, kipindi hicho swala ya jeneza ilikua bado haijateremshwa.
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: