Marjaa dini mkuu, kupitia mwakilishi wake Muheshimiwa Sheikh Abdul-Mahdi Karbalai, amewapongeza mashujaa wema katika makundi yao yote na majina yao yote, kwa mafanikio yao ya kuvutia na ushindi wao muhimu waliouandika kwa damu zao njema, na kwa mihanga yao mikubwa waliyoitoa. Na kwamba wao ndio wanaostahiki zaidi kuliko wengine, kunyanyua bendera ya ushindi wa mwisho. Aidha amebainisha kwamba miaka mitatu iliyotangulia imethibitisha uimara wa wananchi wa Iraq na jinsi walivyojiandaa kwa kiwango cha juu kujitoa muhanga na fidia katika njia ya heshima na utukufu wa taifa lao, endapo kutakuwa na haja ya kujitolea.
Maelezo hayo yamekuja katika hotuba ya pili ya Swala ya Ijumaa ya mwezi 5 Shawwal 1438 Hijiriya, sawa na tarehe 30 Juni 2017 Miladiya, Swala iliyoswaliwa ndani ya ukumbi wa haram ya imamu Hussein (a.s) chini ya uimamu wake, ambapo Muheshimiwa Sheikh Karbalai alisema:
Enyi mabibi na mabwana! Nitawasilisha mambo mawili yafuatayo katika masikio yenu:
Jambo la Kwanza: Wapiganaji wetu mashujaa, katika vita wanavyopigana huko Mosul wameongeza ushindi mwingine wa kipekee katika daftari la kumbukumbu za ushindi mkubwa wa Iraq. Baada ya kupita miezi tisa ya mapambano makubwa, na katika mazingira magumu sana yaliyotengenezwa na sababu mbalimbali, ya muhimu zaidi ikiwa ni kitendo cha maadui kuwatumia raia wa maeneo husika kwa kuwafanya ngao na deraya za kivita, juhudi za wapiganaji hao zimezaa matunda kwa kufanikisha hatua nyingine muhimu miongoni mwa hatua za ushindi wa Wairaq dhidi ya magaidi wa DAESH. Na kutokana na mafanikio haya, tunatoa pongezi na hongera kwa mashujaa hawa wema kwa mafanikio yao ya kuvutia na ushindi wao muhimu. Tunawashukuru wao kuanzia viongozi hadi wapiganaji, kwa juhudi zao kubwa na kwa kujitolea kwao kukubwa katika njia ya kufanikisha ushindi huo. Tunawaombea rehema wale walio mashahidi wema, na tunawaombea ponyo ya haraka wale waliojeruhiwa. Na tunapenda kusisitiza kwamba mtu mwenye fadhila ya kwanza na ya mwisho katika mafanikio haya ambayo mpaka leo hii yamepitiwa na miaka mitatu, ni wale wapiganaji mashujaa walio katika sifa zao na majina yao mbalimbali, kuanzia vikosi vya kupambana na ugaidi, askari wa jeshi la muungano, vikosi vya jeshi la Irak, vikosi vya anga, makundi ya wanamgambo wa kujitolea na wanamgambo wa koo za Wairaki, bila kuzisahau familia zao, koo zao na wale wenye kuwaunga mkono na kuwasaidia. Na hakika hawa ndio wenye ushindi huu waliouandika kwa damu zao njema na kwa muhanga wao mkubwa. Na hakika wao ndio wanaostahiki zaidi kuliko wengine, kunyanyua bendera ya ushindi wa mwisho unaotarajiwa kupatikana muda si mrefu kwa idhini ya Allah, kwa kuyakomboa maeneo mengine yaliyobakia ambayo bado yangali chini ya udhibiti wa makundi ya kigaidi ya DAESH.
Hakika safari ya miaka mitatu iliyopita imefichua kwa uwazi kwamba maadui kama watafanikiwa angalau kwa muda mchache kutimiza malengo yao mabaya katika maeneo ya ardhi safi ya Irak, basi kutokana na misingi ya wananchi wa Irak, maadili yao na hali ya kukataa udhalili na uduni waliyonayo, kamwe hawataweza kukubali kuona hilo, bali watatoa kila lililo ghali na la thamani, na hakuna lililo ghali na thamani kushinda damu yao safi, katika kuhami na kuitetea ardhi yao, heshima yao na matukufu yao. Na miaka mitatu iliyopita imethibitisha uimara wa wananchi wa Irak, na jinsi walivyojiandaa kujitoa muhanga na fidia katika njia ya kulinda heshima yao na utukufu wao pindi haja inapowahitaji kufanya hivyo. Na kwamba wana akiba ya wanamume mashujaa na wanawake imara inayotia matumaini ya kuweza kuvuka majaribu, changamoto, matatizo na mambo magumu yanayoishambulia nchi. Na hivyo ni juu yetu sote kushirikiana nao ili kutimiza malengo yanayokusudiwa kwa ajili ya mustakabali ambao utakuwa na amani, raha, maendeleo na ustawi inshaallah.
Jambo la pili: Enyi mabibi na mabwana! Tunazungumzia utaratibu wa kuishi pamoja kijamii kwa usalama na kwa usahihi ndani ya jamii yenye mirengo tofauti ya kimadhehebu. Kama mnavyojua ndugu zangu, kwamba jamii yetu na pia jamii nyingine nyingi za Kiislamu, zinaishi katika mazingira yenye milengo tofauti ya kimadhehebu na kidini, ndani ya nchi moja. Na hapana shaka kwamba tofauti hii inatokana na kutofautiana itikadi na maarifa, na pia ni kutokana na kutofautiana mambo ya kijamii na kisiasa, na kila mmoja ana utambulisho wa kimadhehebu na kidini. Na tofauti hii inaweza kuzalisha na kuanzisha baadhi ya mambo hasi ambayo tunahitaji kuyatatua. Tofauti hii inaweza kuathiri kwa athari hasi mshikamano na ukaribu wa kijamii na pia mahusiano ya kijamii yaliyopo ndani ya jamii moja ndani ya nchi moja. Na hayo yanaweza kuharibu na kuondoa usalama wa maisha ya kijamii ya kuishi pamoja, hali ambayo kama haitatatuliwa inaweza kuipeleka jamii iliyomo ndani ya nchi moja kwenye ugomvi wa kimadhehebu na wa kidini. Na hivyo hapa tunahitaji kuweka utaratibu wa kifikra na kitamaduni, kijamii na kisiasa, ambao utatuwezesha kuvuka na kukwepa athari hizi hasi zitokanazo na tofauti hii. Hapa tunaweka kanuni na misingi ambayo tunaihitajia katika mfumo wa kiitikadi na kifikra, kanuni ambazo zitatuwezesha kuvuka na kukwepa athari hizi hasi, hivyo hapa kuna mambo matatu ambayo ni lazima tuwe nayo ili tuweze kutatua tatizo hili…