Hivi ndio alivyo uawa imamu Swadiq (a.s)..

Maoni katika picha
Hakika kuuawa kwa imamu Swadiq (a.s) lilikua ni tukio kubwa lililo tikisa ulimwengu wa kiislamu wa zama zile, nyumba za bani Hashim zikapaza sauti pamoja na za watu wengine, watu wakamiminika katika nyumba ya Imamu ambaye alikua kimbilio la waislamu wote.

Mwezi 25 Shawwal 148h Ahlulbait (a.s) na wapenzi wao walipata pigo la kuondokewa na Imamu Jafari bun Muhammad Swadiq (a.s), ambaye ni imamu wa sita katika maimamu watakasifu wa nyumba ya Mtume (a.s).

Kuna riwaya za kuaminika zinazo sema kua Abuu Abbasi Saffaah ambaye ni khalifa wa kwanza wa Bani Abbasi, alitaka imamu aondoke Madina na kwenda Iraq, lakini alishindwa kulazimisha swala hilo baada ya kushuhudia miujiza ya Imamu, elimu kubwa aliyo kua nayo na tabia njema ya hali ya juu kabisa.

Habari zilipo fika kwa Mansour Dawaniqi ndugu wa Saffaah, akaangalia wingi wa wafuasi na wapenzi wa imamu Swadiq (a.s), alikusudia kumwita Iraq kwa lengo la kumuua zaidi ya mara tano lakini aliahirisha kila mara baada ya kuona miujiza mikubwa kutoka kwa Imamu (a.s).

Mitihani ilifululiza kwa mjukuu wa mtume imamu Swadiq (a.s) katika zama za Mansour Dawaniqi, alikua anamwita mara kwa mara na kumtukana pamoja na kumpa vitisho mbalimbali, hakuheshimu elimu, umri, uchamungu na umashuhuri mkubwa alio kua nao Imamu (a.s), Twaghuti huyu (Mansour) hakujali mambo yote hayo, bali aliona imamu ni tishio kwake.

Mansour aliazimia kumuangamiza Imamu kwa hali yeyote ile, akamuandalia sumu kali na akampa mtumishi wake ili amnyweshe, imamu (a.s) alipo kunywa sumu ile, maini yake yalikatika katika na akahisi maumivu makali sana, akatambua kua mwisho wa uhai wake umekaribia.

Mauti yakaja haraka kwa mjukuu wa Mtume, katika dakika za mwisho za uhai wake akaanza kuwahusia watu wa nyumbani kwake kuhusu kupambika na tabia njema, na akawatahadharisha kwenda kinyume na amri za Mwenyezi Mungu na hukumu zake, kisha akaanza kusoma sura za Qur’an tukufu na baadhi za aya, halafu akamuangalia jicho la mwisho mtoto wake imamu Mussa Alkaadhim (a.s), roho yake tukufu ikatoka na kuelekea kwa Mola wake tarehe (25 Shawwal 148h).

Imamu Mussa Alkadhim (a.s) huku akiwa na huzuni kubwa, alianza kuandaa mwili wa baba yake, akamuosha na kumvisha sanda ya pande mbili za vitambaa alivyo kua akifanyia Ihraam, na akamvisha kanzu na kilemba cha babu yake imamu Zainul-abidina (a.s), kisha akamzungushia shuka aliyo inunua imamu Mussa (a.s) kwa dinari arubaini, baada ya kumaliza kumuandaa imamu Mussa (a.s) akaongoza swala ya jeneza iliyo hudhuriwa na mamia ya waisilamu.

Ukabebwa mwili huo mtukufu huku zikisomwa Takbira na watu wakiangua vilio, wakikumbuka utukufu wa imamu katika umma huu, kutokana na namna aliyo unawirisha kwa elimu yake kubwa iliyo gusa kila sekta, mwili huo mtukufu ukapelekwa hadi katika makaburi ya Baqii, akazikwa katika makaburi hayo jirani na kaburi la babu yake imamu Zainul-abidina na baba yake imamu Muhammad Al-baaqir (a.s).
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: