Misingi ya kuishi kwa amani iliyo wekwa na Marjaa dini mkuu..

Maoni katika picha
Marjaa dini mkuu kufuatia mazingira inayo pitia Iraq, ambayo yanapitiwa na hatari nyingi za kiusalama, na kwa ajili ya kuhakikisha nchi inavuka salama katika njama za maadui wanaotaka kuwachonganisha raia wa Iraq, na kusimama pamoja kama jamii moja yenye mshikamano, na kuishi kwa amani na usalama, katika khutuba ya Ijumaa ya leo iliyo tolewa na Muheshimiwa Shekh Abdulmahdi Karbalai, ameelezea misingi ya kuishi kwa amani na akasisitiza ndio njia salama ya itakayo waweka pamoja watu wenye madhehebu, dini na tamaduni tofauti. Misingi yenyewe ni:

Msingi wa Kwanza: Hakika mambo ya ushirikiano yaliyopo baina ya madhehebu za Kiislamu, sawa iwe upande wa itikadi (Tauhidi, unabii na marejea), au upande wa matendo ya kidini ya dini tukufu ya Uislamu, kuanzia Swala, Swaumu, Hija na mengineyo, pamoja na uwepo wa tofauti ndogondogo za hapa na pale katika mambo hayo, lakini mambo hayo yanalazimisha mshikamano wa kitamaduni na mazungumzo yenye kujengeka juu ya msingi wa kuheshimu mambo makhususi ya upande wa pili. Kwa namna ambayo italinda umoja wa kitaifa, ambao ni jambo la ushirikiano baina ya wafuasi wa madhehebu hizi. Na kwa namna ambayo italinda maslahi makuu ya Waislamu wote, hasa wanapokuwa ndani ya nchi moja.

Msingi wa Pili: Kupendana na kuonesha hisia za upendo na huruma na mawada yaliyofaradhishwa na hadithi tukufu: “Mfano wa Waislamu katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao…” hakika hadithi hii imefaradhisha kiwango na daraja ya juu ya kupendana itakayozaa msukumo chanya wa kijamii kuelekea upande wa pili, kwa namna ambayo italinda na kuhifadhi nguvu ya mahusiano ya kijamii. Na kuzuia kiwango cha mtengano na mfarakano kutokuwa juu ya kiwango cha mshikamano na ukaribiano hai wa kijamii.

Msingi wa Tatu: Kuamini kwamba wingi wa dini na madhehebu ni jambo lililopo lisiloepukika, na limepitishwa na utashi wa Mungu “Na laiti Allah angetaka basi angekufanyeni umma mmoja”, hivyo kuishi pamoja kwa amani ni jambo la lazima linalofaradhishwa na uhalisia uliopo na ukweli wa kihistoria. Na hivyo inapasa kujua jinsi ya kuamiliana na wingi wa dini kwa namna itakayoleta matokeo chanya yenye kujenga. Ambayo yatailinda jamii yenye mchanganyiko wa madhehebu isiweze kudumbukia katika mizozo na matumizi ya nguvu. Na jambo linalotakiwa ni kuamiliana na wingi wa dini kwa kutumia akili, uhalisia na uadilifu.

Msingi wa Nne: Hakika miongoni mwa haki za kila mwenye fikra ni kuitetea fikra yake na kujaribu kutaka kuwakinaisha wengine kwa kutoa dalili, na kwa kufuata njia za kielimu katika kuthibitisha jambo ambalo kwa mtazamo wake ni haki. Lakini bila kuvunja heshima za wanaomkhalifu katika fikra, na bila kujeruhi hisia zao na bila kuyavunjia heshima matukufu yao kwa mambo ambayo yanaweza kuondoa na kuvuruga hali ya kuishi pamoja kwa amani baina ya watu wa nchi moja. Kusudio hapa si kwamba mwenye haki asitangaze na kubainisha lile lililo haki na watu wake, au lile lililo batili na watu wake, lakini ni lazima kufuata njia sahihi katika hilo, na kujiepusha na mambo yanayoleta hikdi na chuki baina ya watu.

Msingi wa Tano: Hakika miongoni mwa mambo hatari ambayo yamesababisha umwagaji mkubwa wa damu za watu wasio na hatia, ni suala la kuwakufurisha wengine kwa kuwa tu mtu anatofautiana nao katika baadhi ya mambo ya kiitikadi. Ikiwemo pia suala la kuzitafsiri nususi kwa maana isiyo ile iliyokusudiwa, hasa zile nususi zilizolinda na kuhifadhi jamii ya Kiislamu upande wa damu za watu wake, heshima yao na mali zao.

Msingi wa Sita: Hakika kutambua yale yatokanayo na maslahi makuu ya Waislamu, na maslahi ya umma ya kitaifa, ni jambo muhimu zaidi kuliko maslahi finyu ambayo baadhi ya watu wanadhani kuwa ni maslahi ya madhehebu na kundi. Hivyo inatakiwa kuheshimu haki za kitamaduni, kiuchumi na kijamii za watu wote ndani ya duara la haki za raia ambazo katika haki hizo watu wote wako sawa. Na kuishi kwa kuzingatia kanuni ya misingi na maslahi ya pamoja, na kutupilia mbali uharibufu utokanao na mfarakano na mpasuko wenye kuwadhuru wote.

Msingi wa Saba: Hakika miongoni mwa mambo yanayoteteresha hali ya kuishi pamoja kwa amani, ni kukithiri kwa mijadala na ubishi na kuwakosoa wengine katika mazungumzo ya jumla. Aidha ni kujitenga na njia ya uwasilishaji wa kielimu ndani ya duara la wabobezi na wenye jukumu la kufikisha kwa njia ya Uislamu, na kwa ubainifu wa mambo ya haki. Hivyo atakayeamini atakuwa ameitendea wema nafsi yake, na asiyeamini hisabu yake ni kwa Allah Mtukuka “Hakika ni juu yako kufikisha, na ni juu yetu hisabu.”
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: