Msimu wa hija katika mwaka wa 60 hijiriyya sawa na 679 miladiyya, Imamu Hussein (a.s) aliondoka Makka na kuelekea katika mji wa Kufa, aliondoka maka siku ya Tarwiyya, mwezi nane Dhulhijjah, msafara huo; Uliojaa utukufu, ulikua na vituo vingi, kituo cha mwisho kikawa ni katika aridhi tukufu ya Karbala, Imamu (a.s) akauliza, (kanakwamba alikua anatafuta aridhi ya Karbala), akasema: “Hii aridhi inaitwaje?” akaambiwa: Aridhi ya Twafu. Akauliza tena (a.s): “Je! Inajina lingine tofauti na hilo?” akaambiwa: Jina lake lingine inaitwa Karbala. Akasema (a.s): “Ewe Mola najilinda kwako kutokana na matatizo na balaa”.
Kisha akasema (a.s): “Hii ni sehemu ya matatizo na balaa, telemkeni, hapa ndio kituo cha msafara wetu, na sehemu zitakapo mwagika damu zetu, hapa ndio sehemu ya kaburi zetu, hivi ndio alivyo nihadithia babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) telemkeni wote”.
Siku aliyo wasili Imamu (a.s) katika aridhi ya Karbala ilikua ni mwezi pili Muharam mwaka wa sitini na moja hijiriyya, kwa mujibu wa riwaya nyingi zinasema ilikua siku ya Alkhamisi, ndiyo alifika Imamu Hussein (a.s) katika aridhi wa Karbala, akafunga hema zake na akaanza kurekebisha siraha yake huku akisoma beti zifuatazo:
Ewe dahari koma kwa kipenzi*** mara ngapi umechomoza na kuzama.
Kwa rafiki au (adui) mtafuta kifo*** na dahari haitosheki kwa kidogo.
Hakika (maamuzi) amri ni ya Jalali*** kila aliye hai atapita katika njia.
Bibi Zainab (a.s) alipo sikia beti hizo, akasema: “Ewe kaka yangu! Haya ni maneno ya mtu mwenye yakini ya kuuawa” akasema (a.s): “Ndio, ewe dada yangu” akasema: “Ole wangu, hili jambo ni zito kwangu”.
Mahema ya Imamu Hussein (a.s) yaliwekwa katika aridhi hiyo ambayo bado athari yake ipo hadi leo, sehemu hiyo ilikua mbali kidogo na maji, lilifungwa hema la Imamu Hussein (a.s) likazungukwa na mahema ya watu wa familia yake kisha yakafungwa mahema ya maswahaba zake.