Baada ya kuisha vita ya Twafu, Omari bun Saadi bun Waqaas aliamuri kukatwa kicha cha Imamu Hussein (a.s) na vichwa vya watu wa nyumbani kwake (a.s), pamoja na vichwa vya maswahaba wake watukufu, kwa hiyo maiti zikakatwa vichwa na makabila yaliyo shiriki katika mauaji hayo, yakavigawana vichwa vya mashahidi, ili kupitia vichwa hivyo wajikurubishe kwa bun Ziyadi, siku ya mwezi kumi na moja Omari bun Saadi na wanajeshi wake, walishinda wanakusanya miili ya watu wake waliokufa, akawaswalia na kuwazika, ilipo fika jioni wakaondoka kuelekea katika mji wa Kufa wakiwa wamebeba vichwa vya mashahidi walio uawa upande wa Imamu Hussein (a.s), pamoja na mateka ambao ni wanawake na watoto wa nyumba tukufu ya Mtume (s.a.w.w), na akaacha miili ya mashahidi hao watukufu imelala aridhini bila kuzikwa.
Msafara uliwasili katika mji wa Kufa mwezi kumi na mbili Muharam, watu wa kufa wakashangaa, wakasimama njiani wakiwa baadhi yao hawajui nini kimetokea, na wanaojua wanalia na wamejaa huzuni.
Msafara wa mateka ukaelekea katika jumba la ikulu (utawala), ukipita katikati ya makundi ya watu wa Kufa wanaolia kutokana na kuuliwa kwa watu wa familia ya Mtume mtukufu, na kuvunja ahadi zao kwa mjukuu wa Mtume (s.a.w.w) Imamu wa waislamu Hussein (a.s), sasa wanaona familia yake, wanawake na watoto wakiwa mateka, na kichwa cha mjukuu wa mtume kimetungikwa katika mikuki na kuzungushwa katika njia za Kufa, wakati walimwita awe kiongozi wa Umma wa kiislamu na awaelekeze katika usawa.
Bibi Zainabu (a.s) aliwaangalia watu wa Kufa, akiwa na hasira ya kuuliwa kwa kaka yake pamoja na udhalili wanao fanyiwa, akawaambia kwa hasira: (Ole wenu enyi watu wa Kufa.. hivi mnajua ubaya gani mmemfanyia Mtume wa Mwenyezi Mungu? Na kwa kiasi gani mmemvunjia heshima yake? Kwa kiasi gani mmemwaga damu yake? Kwa kiasi gani mmevunja heshima yake? Hakika mmefanya jambo baya mmno, Mbingu zinakaribia kupasuka kwa jambo hilo, Aridhi inakaribia kupasuka na milima kung’ooka).
Kichwa cha Imamu Hussein (a.s) kikaingizwa katika jumba la mfalme, kikawekwa mbele ya bun Ziyadi, akaanza kukipiga piga kwa fimbo yake aliyo kua nayo mkononi, akionyesha furaha kubwa, kisha wakaingizwa mateka, wanawake na watoto pamoja na Ali bun Hussein (a.s), bun Ziyadi akaanza kumshtum bibi Zainabu (a.s), kwa kumuambia kua: (Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu ambaye amekufedhehesheni, kawauweni na kakadhibisha mambo yenu). Bibi zainabu akamjibu kwa ujasiri: (Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu ambaye ametukirimu kwa kutuletea mtume Muhammad (s.a.w.w), na ametutakasa kutokana na uchafu, hakika huwafedhehesha mafasiki na huwakadhibisha waovu).
Bun Ziyadi akasema: Umeonaje Mwenyezi Mungu alivyo wafanya watu wa nyumbani kwako?
Bibi Zainabu akajibu: (Mwenyezi Mungu aliwaandikia kuuawa, wangeuawa hata katika vitanda vyao, na atawakusanya wewe na wao na mtahojiana mbele yake).
Kisha ukaja muda wa Imamu Sajjaad (a.s), akasimama mbele ya Ubaidullahi bun Ziyadi, akamuuliza: Nani wewe? Akamjibu: Mimi ni Ali mtoto wa Hussein (a.s). Bun Ziyadi akasema: Hivi Mwenyezi Mungu hajamuua Ali bun Hussein? Akamjibu kua: Nilikua na ndugu anaitwa Ali bun Hussein ameuliwa na watu. Bun Ziyadi akasema: Bali kauliwa na Mungu, Imamu (a.s) akamjibu: (Mwenyezi Mungu huzipokea roho zinapo kufa), Bun Ziyadi akakasirika, akamwita Jalauza na akamwambia: Kata shingo yake! Bibi Zainabu akamkumbatia Zainul-abidina na akasema (kwa ukali): (Ewe bun Ziyadi! Yatosha kumwaga damu zetu, wallahi simuachii kama mkimuua, mniue pamoja naye) bun Ziyadi akashusha hasira zake.
Roho mbaya ya bun Ziyadi na ukatili wake haukuishia hapo, siku ya pili aliamrisha kichwa cha Imamu Hussein (a.s) kitembezwe katika barabara za Kufa, ili kuwaogopesha wakazi wa mji huo na kuvunja moyo wa upinzani dhidi yake.