Kama kawaida yake katika kila mwaka, kinapo anza kipindi cha ziara ya Arubaini ya Imamu Hussein (a.s), mgahawa wa Atabatu Abbasiyya tukufu uliopo barabara ya (Karbala – Najafu), unafanya hafla ya kupandisha bendera ya utukufu na ukarimu na kutangaza utayari wake wa kuwahudumia mazuwaru (watu wanaokuja kufanya ziara) watukufu, kwa ajili ya kumtambulisha zaairu aliye zowea kuona bendera hii ikipepea juu kila mwaka katika eneo hili la mgahawa.
Shughuli hii imefanywa asubuhi ya leo (29 Muharam 1439h) sawa na (21 Oktoba 2017m) katika uwanja wa mgahawa na kuhudhuriwa na kiongozi mkuu wa kisheria katika Atabatu Abbasiyya tukufu, Muheshimiwa Sayyid Ahmad Swafi na katibu mkuu Muhandisi Muhammad Ashiqar pamoja na jopo la viongozi wa Ataba tukufu, bila kuwasahau viongozi mbalimbali wa kidini na kikabila pamoja na watu wa usalama na wengineo.
Hafla ilifunguliwa kwa Qur’an tukufu, halafu ukaimbwa wimbo wa taifa na wimbo wa Atabatu Abbasiyya tukufu.
Halafu ukafuata ujumbe wa uongozi mkuu wa Atabatu Abbasiyya tukufu, ulio wasilishwa na Sayyid Adnaan Mussawiy kutoka katika kitengo cha dini, alizungumzia mambo yaliyo jiri katika vita ya Twafu ikiwa ni pamoja na kurejea kwa bibi Zainabu (a.s) katika kaburi la kaka yake Imamu Hussein (a.s) katika siku ya Arubaini, akakumbusha athari iliyo patikana kutokana na tukuo hilo, akasema kua: “jana ilibadilishwa bendera nyekundu na kuwekwa bendera nyeusi katika malalo ya Abuu Abdillah Hussein na ndugu yake Abulfadhil Abbasi (a.s), na jambo hili limekua likifanyika kila mwaka, na leo inapandishwa bendera nyingine katika mgahawa miongoni mwa migahawa ya Abulfadhil Abbasi (a.s), huu ni mgahawa wa kwanza kupandisha bendera kubwa ya aina hii, nawapongeza sana walio anzisha jambo hili jema, bendera hii ni ishara ya ushindi wa Bwana wa Mashahidi na maswahaba wake watakatifu hususan mmbeba bendera wake na msaidizi wake Abulfadhil Abbasi (a.s), hili ni jibu kwa wale wanaotaka kuzima nuru ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anakataa jambo hilo lazima idhihiri nuru yake”.
Akaongeza kusema kua: “Kuna walio mbeba Imamu Hussein (a.s) katika nyoyo zao na wakajifananisha na maswahaba wake, jambo hilo tumeliona kwa wapiganaji wetu watukufu, walio itikia wito wa Marjaa dini mkuu na wakajitolea damu zao tukufu kwa ajili ya kulinda taifa hili na maeneo yake matukufu, kwa kujitolea kwao watakutana na mashahidi wenzao watakatifu wakiwa wameloa damu zao”.
Naye Hamid Tamimiy akasoma mashairi ya maombolezo yaliyo elezea kurudi kwa msafara wa mateka katika aridhi ya Karbala yaliyo tia huzuni na majonzi katika nyoyo za wapenzi wa Ahlulbait (a.s).
Kisha wahudhuriaji wakaelekea katika shughuli ya kupandisha bendera ya utukufu na ukarimu, na kuanza kupepea katika anga la Karbala kana kwamba ni mkono wa Abulfadhil Abbasi (a.s) ukiwakaribisha watu wanaokuja kufanya ziara na kuwaambia ingieni Karbala kwa amani na salama.
Kumbuka kua bendera imepandishwa katika nguzo yenye urefu wa mita 40, upana wa bendera ni mita 13 na ina urefu wa mita 17 imeandikwa pande zote mbili maneno yasemayo: (Salaamu alaika yaa haamilu liwaai Hussein alaihi salaam)