Kituo cha afya kilicho chini ya Atabatu Abbasiyya tukufu pamoja na udogo wa eneo lake, kinatoa huduma kubwa za matibabu na vipimo, kinafanya hivyo mwaka mzima, lakini kipindi cha ziara ya Arubaini kazi zake huongezeka maradufu, hufanya kazi kutokana na wingi wa mazuwaru wanaokuja kumzuru Imamu Hussein na ndugu yake Abulfadhil Abbasi (a.s), kituo hiki kinafanya kazi kwa kufuata utaratibu ulio wekwa na Atabatu Abbasiyya na kwa kushirikiana na ofisi ya afya ya mkoa mtukufu wa Karbala.
Mganga msaidizi Yusufu Twalibu Kadhim amesema kua: “Tumechukua tahadhari zote za lazima kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa mazuwaru,katika upande wa wahudumu, tumeongeza wahudumu ambao ni watalamu wa fani mbalimbali (wanaume na wanawake) kutoka idara ya afya ya mkoa wa Karbala pamoja na madaktari wa kujitolea, na tuliweka umuhimu zaidi katika kupata madaktari wa presha (shindikizo la damu), kifua, tumbo pamoja na magonjwa mengine”.
Akaongeza kua: “Tumesambaza gari za wagonjwa katika maeneo mbalimbali, ambazo huleta wagonjwa katika kituo hiki au hupeleka katika hospitali tulizo fanya nazo makubaliano maalumu, ambazo ni; hospitali ya Safiir na hospitali ya Imamu Hussein (a.s), na kazi ya matibabu inafanyika saa 24”.
Tunapenda kufahamisha kua; Idara ya afya ya mkoa wa Karbala kwa kushirikiana na vituo vya afya vya Ataba mbili tukufu (Husseiniyya na Abbasiyya) pamoja na vituo vingine vya afya, wamejipanga kutoa huduma bora za matibabu kwa mazuwaru watakao pata maradhi kipindi cha ziara ya Arubaini, pia wamewasiliana na idara za afya za Najafu na Baabil ziandae jopo la madaktari wa dharura. watakao kua tayari kutoa huduma wakati wowote watakapo hitajika.