Watumishi wa Imamu Hussein (a.s) waliopo katika njia wanazo pita mazuwaru watukufu wanaokwenda Karbala kufanya ziara ya Arubaini, wanajitahidi kutoa kila aina ya huduma katika mawakibu zao, mara hii wahudumu wa maukibu ya bibi Ruqayya katika barabara ya (Hilla – Karbala), wanatoa huduma ya kuosha miguu ya mazuwaru na kuifunga bandeji, baada ya kua mazuwaru hao wametembea kwa miguu mamia ya kilo meta wakielekea Karbala kutoka katika miji tofauti.
Katika maukibu hii, zaairu (mtu) anapata huduma inayo mpunguzia maumivu ya miguu aliyo nayo kutokana na kutembea umbali mrefu.
Muoshaji anakaa chini ya kiti na muoshwaji anakaa juu ya kiti, kisha muoshaji anaanza kusafisha miguu kwa maji hadi inatakata kabisa kisha anaikandakanda kwa dawa halafu anaifunga bandeji.
Makumi kwa mamia ya mazuwaru wanapo fika katika maukibu hii wanapenda kufanyiwa huduma hiyo, na mawakibu zingine zimeanza kutoa huduma sawa na hiyo, pia vituo vya afya vimejaa njia nzima.
Huduma hii sio mpya, maukibu hii na zingine hutoa huduma hii kila mwaka kwa watu wanaokuja kufanya ziara katika kaburi la Imamu Hussein na ndugu yake Abulfadhil Abbasi (a.s).
Kutokana na kukaribia kilele cha ziara ya Arubaizi mwezi Ishirini Safar, miji ya kusini imebaki mitupu baada ya wakazi wake kuelekea Karbala kushiriki katika ibada ya ziara.