Mwezi nane Rabiul-Awwal ni kumbukumbu ya kuawa kishahidi kwa Walii wa Mwenyezi Mungu Imamu Hassan Askariyyu (a.s)…

Maoni katika picha
Mwezi nane Rabiul-Awwal inasadifu siku aliyo uawa kishahidi mwezi wa kumi na moja miongoni mwa miezi ya watu wa nyumba ya Mtume ambaye ni Imamu Abu Muhammad Hassan bun Ali bun Muhammad bun Ali bun Mussa bun Jafari bun Muhammad bun Ali bun Hussein bun Ali bun Abu Twalib (a.s), na alipewa jina la sifa (laqabu) la Askariyyu, Siraaju, Khaalisu, Swaamit, Taqiyyu, Zakiyyu, Naqiyyu… anajulikana zaidi kwa jina la Askariyyu.

Siku za uhai wake alizimaliza katika mitihani, alipambana na dhulma za wafalme wa bani Abbasi kwa subira yake, walikuwa wanamuhamisha gereza moja hadi lingine, walimzuia kuonana na wafuasi wake, pia waliwazuia wanachuoni na maulamaa kwenda kusoma kwake, huo ni mtihani mkubwa alio upata.

Alizaliwa Rabiu-Thani mwaka wa 232h na akauawa mwaka wa 260h akiwa na umri wa miaka 28 tu, yeye na babu yake Imamu Jawaad ni Maimamu walio fariki wakiwa na umri mdogo zaidi, Imamu Jawaad alifariki akiwa na umri wa miaka 25.

Aliitwa Askariyyu kutokana na jina la mahala alipokua anaishi pamoja na baba yake Imamu Haadi (a.s) katika mji wa Samara (kaskazini ya Iraq), alilelewa na baba yake aliye julikana zaidi kwa elimu, uchamungu, jihadi na matendo mema, akajifunza kutoka kwa baba yake tabia njema na ubobezi wa elimu, aliishi pamoja na baba yake miaka ishirini na tatu na miezi kidogo, katika kipindi hicho alipata elimu ya maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w), alipo chukua rasmi madaraka ya uimamu alikua sawasawa na baba zake kielimu, kiuchamungu na kulingania maelewano katika umma wa babu yake Muhammad (s.a.w.w).

Imamu Hassan Askariyyu (a.s) alichukua rasmi madaraka ya uimamu mwaka wa 253h baada ya kufariki baba yake, utawala wa bani Abbasi haukuacha kumuandama, walimuweka chini ya kizuizi kikali, walidhibiti harakati zake na wakamtenga na wafuasi wake…

Imamu alitumia njia ya siri katika kufikisha ujumbe na kuwajenga wafuasi wake bila viongozi wa bani Abbasi kujua, vitabu vya historia vimeelezea njia makini aliyo itumia Imamu (a.s).

Imamu Hassan Askariyyu (a.s) alikutana na mitihani kama waliyo kutana nayo baba zake (a.s), mitihani ya kisiasa na kupambana na dhulma na ugaidi, na kulinda misingi sahihi ya ujumbe wa uislamu ambalo ndio jukumu lao la msingi walilo pewa na Mwenyezi Mungu mtukufu, katika kutekeleza jukumu hilo walipatwa na matatizo mengi ya muda mrefu, walifungwa jela walinyanyaswa na kuuawa.

Imamu aliishi katika zama za watawala watatu wa bani Abbasi ambao ni; Mu’taz, Muhtada na Mu’tamad, wote hao walimdhalilisha na kumtesa, walimkamata mara kwa mara na kumuweka kizuizini, na wamwisho wao ambae ni Mu’tamad, alikua anapenda ufuska, miziki na kufanya mambo ya haram, watu wote walichukizwa na vitendo vyake, mtawala huyo alimbana sana Imamu, alimuweka katika kizuizi kikali na akapiga marufuku kuwasiliana na mtu yeyote.

Kilicho sababisha viongozi wa bani Abbasi kumdhibiti Imamu Hassan Askariyyu (a.s) kiasi hicho, kwanza walikua wanahofia haiba yake na kukubalika kwake kwa watu, pili walikua wanaogopa kuzaliwa kwa Imamu Mahdi Msubiriwa (Almuntadhir) –a.f-, kwani walikua wanajua kua atazaliwa na Imamu Hassan Askariyyu.

Hivyo Mu’tamad akampa sumu kali Imamu (a.s) iliyo mtesa siku kadhaa na hatimae akafariki dunia, alifariki mwaka wa 260h akiwa na umri wa miaka ishirini na nane.

Alizikwa pamoja na baba yake Imamu Haadi (a.s) katika nyumba yake Samara, sehemu ambapo lipo kaburi lake hadi leo, watu kutoka kila kona ya dunia huenda kulizuru, na wapenzi wa watu wa nyumba ya Mtume watakasifu hutabaruku kwalo na humuomba Mwenyezi Mungu mtukufu awaingize katika rehma zake na awaongoze katika haki kwa utukufu wa walio zikwa hapo.
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: