Maana ya kutawazwa na miaka yake:
Mwezi tisa Rabiul-Awwal 260h, ndio siku aliyo tawazwa Imamu Mahdi (a.f), alishika madaraka rasmi ya uimamu akiwa na umri wa miaka mitano, baada ya kufariki baba yake Imamu Hassan Askariyyu (a.s), hivyo yeye ndiye mtu aliye pata uimamu akiwa na umri mdogo zaidi, zimepokelewa hadithi nyingi zikielezea swala hilo kutoka kwa maimamu watakasifu (a.s).
Jambo hili sio jipya katika historia ya Manabii, Mitume na Maimamu wa Ahlulbait (a.s), wapo mitume walio waliokua na umri mdogo kama inavyo sema Qur’an tukufu, hali kadhalika kulikua na maimamu wenye umri mdogo, kama vile Imamu Haadi (a.s), alipata uimamu akiwa na miaka nane, na Imamu Jawaad (a.s) alipata uimamu akiwa na miaka saba au tisa.
Hakika udogo wa umri hauathiri chochote katika kazi ya Mwenyezi Mungu anapo panga jamo fulani kwa mja wake, ndio maana utaona walio andika kuhusu Uimamu wa Mahdi (a.s) waliona kupata kwake uimamu akiwa na umri mdogo (miaka mitano) ni jambo la kawaida katika sira ya Maimamu (a.s), ibun Hajari Haithamiy Ashafiiyyu Almakiyyu ameandika kuhusu Imamu Hassan Askariyyu kua: (Hakuacha kiongozi mwingine (Imamu Hassan Askariyyu) ispokua mwanae Abu Qassim Muhammad Alhujjah (a.s) akiwa na umri wa miaka mitano makati wa umauti wa baba yake).
Kusherehekea tukio hili:
Wapenzi na wafuasi wa Ahlulbait (a.s) katika siku kama hii huonyesha furaha na hufanya mahafali, kwani ndio siku ya kwanza ya uongozi wa muokozi wa wanadamu, na Imamu wa mwisho (a.s), kutokana na mnasaba huu tunamuomba Mwenyezi Mungu mtukufu aharakishe kumrudisha Imamu wetu mtukufu (a.s) aje kujaza dunia amani na uadilifu kama ilivyo bashiriwa na babu yake Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika hadithi mutawatira zilizo ripotiwa na vitabu vya waislamu.
Aamali na adabu za siku ya kutawazwa kake:
Katika siku hii tukufu tunatoa pongeza kwa Swahibu Asri wa Zamaan na bibi yake mtakasifu Zaharaa (a.s).
Katika siku kama ya leo inapendekezwa kutoa sadaka na kugawa chakula, imepokewa katika riwaya kua: (Atakaetoa kitu chochote katika siku kama ya leo Mwenyezi Mungu atamsamehe dhambi zote), na imesuniwa kuvaa nguo mpya, na kushukuru na kufanya ibada, nayo ni siku ya kuondoa majonzi na huzuni.
Imesuniwa pia kumzuru Imamu Mahdi (a.f) na kusoma surat Swafaat na kuelekeza thawabu zake kwa mama wa Imamu Mahdi (a.f).
Mtume (s.a.w.w) aliulizwa kuhusu namna ya kunufaika na Imamu Mahdi (a.s) katika kipindi cha ghaiba (maficho) yake, akasema: (Naapa kwa ambaye amenifanya kua Mtume, hakika watu wataangaziwa na nuru yake na kunufaika na uongozi wake wakati wa ghaiba (maficho) yake, kama wanavyo nufaika na jua hata kama likifunikwa na mawingu).
Nini yapasa kufanya katika siku ya kutawazwa kwake?
Katika kumbukumbu hii na katika siku zote za uhai wetu, hua tunamkumbuka Imamu wetu ambaye yupo ghaibu (mafichoni) na tunaendelea kumsubiri kwa vizazi na vizazi, yeye ndiye Imamu aliye ahidiwa kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu na kuweka uadilifu katika aridhi, na kupambana na dhulma, uovu na ufisadi, na kukamilisha ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuufanya uislamu kua juu kuliko dini zingine zote, kama ilivyo kuja katika Qur’an tukufu na katika riwaya za Ahlulbait (a.s).
Yatupasa watu wote tufungamane na Imamu Mahdi (a.f) katika kipindi hiki cha ghaiba yake kubwa, ili ufungamane naye lazima umfahamu vilivyo, kila unapo ongeza uwelewa wako kuhusu Imamu ndivyo utakavyo ongeza kufungamana naye.
Ghaiba ndogo:
Na katika siku kama ya leo, Imamu Mahdi (a.s) alitoweka katika macho ya watu, na ndio ukawa mwanzo wa ghaiba ndogo iliyo dumu miaka sabini.