Katibu mkuu wa Atabatu Abbasiyya tukufu Muhandisi Muhammad Ashiqar ametoa pongezi kwa kila aliye shiriki kuchangia na kujitolea hadi akapata shahada chini ya bendera ya Iraq na kivuli cha fatwa ya Marjaiyya, hali kadhalika ametoa pongezi kwa familia za mashahidi, ameyasema hayo katika ujumbe wake aliotoa kwenye shughuli ya kushindikiza jeneza la kimaigizo iliyo fanyika siku ya Juma Mosi (7 Jamadal-Thani 1439h) sawa na (24 Februari 2018m) chini ya usimamizi wa kitengo cha Mawakibu na vikundi vya Husseiniyya cha Ataba mbili tukufu Husseiniyya na Abbasiyya.
Amesema kua: “Pongezi kwa aliye shiriki, akachangia na akapata shahada chini ya bendera ya Iraq na kivuli cha fatwa adhimu ya kulinda taifa na maeneo matukufu, hongera kwa familia zao na watoto wao kwa utukufu huu mkubwa, wamefuata nyayo za maimamu watakasifu (a.s), napenda kusisitiza kwa mara nyinge umuhimu wa kulinda ushindi na kuhifadhi historia tukufu kwa kuendelea kuwasidia na kuwajali wale walio leta ushindi, kupitia kujitolea kwao na kumwagika kwa damu ya mashahidi wetu (r.a)”.
Akaongeza kusema kua: “Kutoka katika mji wa Karbala, ardhi ya Hussein (a.s), ardhi ya mwenye utukufu wa milele na muendelezaji wa ujumbe wa Utume mtukufu, katika ardhi ya Twafu, Twafu ya ushujaa na kujitolea, kutoka katika ardhi takatifu ilipo tangaziwa fatwa tukufu, fatwa ya Marjaa dini mkuu ya wajibu wa kutoshelezeana (kifai) wa kuilinda Iraq, raia wake na maeneo matukufu, fatwa iliyo itikiwa na watu walio amini mambo waliyo ahidiwa na Mwenyezi Mungu, wakashindana katika kutafuta shahada, wakatengeneza historia sawa na ile ya vizazi vilivyo tangulia, wakaiga mwenendo wa Abul-Ahraar Imamu Hussein (a.s) na ndugu yake Abulfadhil Abbasi (a.s)”.
Akabainisha kua: “Ni jana tu, lilijitokeza kundi la vijana miongoni mwa waumini kwa ajili ya kuilinda ardhi ya Iraq, vijana waliovaa ngao katika nyoyo zao, kutokana na ujasiri mkubwa na nguvu na kutokata tamaa wamefanikiwa kufikia malengo, na wakawa miongoni mwa mashahidi wa mwanzo na sasa tumepata neema ya amani na usalama kutokana na baraka ya kujitolea kwao”.
Akaendelea kusema kua: “Leo tumepata utukufu wa kushindikiza jeneza la kimaigizo la mashahidi wa fatwa tukufu, wapiganaji jasiri kutoka katika vikosi mbalimbali, kuanzia jeshi la kupambana na magaidi, jeshi la umoja, na vikosi mbalimbali vya jeshi ya Iraq, jeshi la anga pamoja na vikosi vya wapiganaji wa kujitolea, na vikosi vya kikabila vilivyo jitolea pamoja na familia zao na kila aliye toa msaada wa hali na mali, kama walivyo orodheshwa na Marjaa dini mkuu katika khutuba yake iliyo tolewa ndani ya ukumbi wa haram tukufu ya Husseiniyya (Kutokana na utukufu wa kujitolea kwao na damu zao takasifu, umepatikana ushindi mkubwa, miji, vijiji pamoja na ardhi yote ya Iraq imekombolewa)”.
Akafafanua kua: “Natoa salamu kwa watukufu hawa ambao Marjaa dini mkuu, amewaita kua ni watu wenye utukufu wa mwanzo na wa mwisho katika eneo hili la ushujaa, watu hawa ambao Mheshimiwa Ayatullah Sayyid Ali Sistani ameandika kwa mikono yake mitukufu kua: (Hakika mashahidi wa fatwa ya kujilinda wana haki kubwa juu yetu sote, na wana nafasi kubwa kwetu, namuomba Mwenyezi Mungu mtukufu awafufue pamoja na Answari wa Hussein (a.s)), maneno haya matukufu yametupa jukumu kubwa raia wote wa Iraq pamoja na wa vizazi vijavyo kuhakikisha tunatekeleza haki hiyo kwa nguvu zote, hakika watu hawa wana nafasi kubwa sana juu yetu, tumesikia mara nyingi kutoka kwa wapiganaji kua walikua wanatamani kupata utukufu wa shahada katika vita, pia tumesikia kutoka kwa ndugu zetu majeruhi (mashahidi hai) wakisema huu ni utukufu mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu juu yetu, na ni fursa kubwa ambayo wazazi wetu hawakuipata kwa muda mrefu, fursa ya kupata shahada kama hivi”.
Tunamaliza kwa kauli ya Marjaa mtukufu: (Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu raia wenye msimamo na subira, mmeishangaza dunia kwa subira yenu na ujasiri wenu).