Imamu Mahdi (a.f) ni Imamu wa kumi na mbili katika Maimamu wa Ahlulbait (a.s), ni mtoto wa tisa katika kizazi wa Imamu Hussein (a.s), alizaliwa katikati ya mwezi wa Shabani mwaka wa 255 hijiriyya, katika mji wa Samara. Amebashiriwa katika riwaya na hadithi kua atajaza dunia haki na uadilifu baada ya kua imejaa dhulma na ufisadi.
Imamu wa Zama anatokana na kizazi cha Imamu Hussein (a.s) naye ni mtoto wa Imamu Ali bun Abu Twalib na bibi Fatuma Zaharaa (a.s), imepokewa katika hadithi: Mtume (s.a.w.w) anasema: [Nakubashiria ewe Fatuma Mahdi atatokana na wewe] akasema tena: [Na miongoni mwetu atatokea Mahdi (muokozi) wa umma ambaye Nabii Issa ataswali nyuma yake –kisha akapiga bega la Hussein- akasema: kutokana na huyu atapatikana Mahdi (muokozi) wa umma]. Katika hadithi nyingine akasema kua: [Mahdi atatokana na Ahlulbait…]. Kutokana na hadithi hizo ni wazi kua Imamu Mahdi ni miongoni mwa Maimamu wa Ahlulbait (a.s) naye ni Imamu wa mwisho katika Maimamu kumi na mbili walio bashiriwa na Mtume (s.a.w.w) pale alipo sema: (Baada yangu watukuja makhalifa kumi na mbili wote wanatokana na Makuraishi), tena katika kizazi kitakasifu cha Fatuma Zaharaa na miongoni mwa wajukuu wa Imamu Hussein Shahidi (a.s).
Bibi Hakima ambaye ni shangazi wa Imamu Hassan Askariy (a.s) anatuhadithia kisa cha kuzaliwa kwa Imamu Mahdi, bibi Hakima alikua kila anapo mtembelea Imamu Askariy (a.s) anamuombea kwa Mwenyezi Mungu apate mtoto wa kiume, anasimulia kua: Niliingia kwake siku moja, nikamuambia kama nilivyo kua nikimuambia na nikamuombea dua ambayo hua namuombea, akasema: ewe shangazi katika nyumba yangu usiku huu atazaliwa mtoto mtukufu mbele ya Mwenyezi Mungu, ambaye Mwenyezi Mungu ataihuisha ardhi baada ya kufa kwake kupitia mtoto huyo, bibi Hakima akauliza, Nani atakaye zaa ewe kiongozi wangu sioni kama Narjisi ana ujauzito? Akasema, Atazaliwa na Narjisi wala sio mwingine, akasema: nikaingia kwa Narjisi nikamgeuza mgongoni na tumboni sikuona dalili za ujauzito, nikarudi kwake nikamuambia nilivyo fanya, akatabasamu kisha akasema: Utakapo fika wakati wa Alfajiri ujauzito wake utadhihiri kwako, mfano wa ujauzito wake ni sawa na ule wa mama yake Nabii Mussa haukuonekana, hakuna aliye jua kama anaujauzito hadi wakati wa kujifungua, kwa sababu Firaun alikua anapasua matumbo ya wajawazito kwa ajili ya kumtafuta Mussa na huyu ni mfano wa Mussa (a.s) (atakuja kumaliza utawala wa kifiraun).
Hakima akasema: Niliendelea kumuangalia usiku mzima akiwa amelala hadi ilipo chomoja Alfajiri, ilipo ingia Alfajiri nikaona dalili za kujifungua, nikamkumbatia, Imamu Askariy (a.s) akaita na akasema: msomee (Innaa anzalnaahu fii lailatil qadri) nikaanza kumsomea, nikamuuliza kuna hali gani? Akasema: kimetokea kile ulicho niahidi ewe kiongozi wangu, nikaendelea kumsomea kama alivyo niambia, kisha nikamsikia mtoto naye anasoma kama ninavyo sama mimi kutokea katika tumbo la mama yake halafu akanitolea salamu, nikashangazwa na nilicho sikia, Imamu Askariy (a.s) akaniita na akasema: Usishangae kazi ya Mwenyezi Mungu mtukufu, hakika humtamkisha mtoto mdogo kwa rehma zake, na kumfanya kua hoja kwa walimwengu anapo kua mkubwa, kabla hajamaliza maneno yake bibi Narjisi akatoweka machoni mwangu kana kwamba baina yangu na yeye kulikua pazia, nikaenda kwa Imamu huku nikiita, akaniambia: rudi ewe shangazi yangu hakika utamkuta palepale, akasema: Nikarudi kisha nikaona kama vile pazia imeondoshwa baina yetu, ikatokea nuru kubwa kisha nikamuona mtoto akiwa amesujudu na ameinua kidole cha shahada huku anasema: (Nashuhudia kua hakuna Mungu ispokua Allah mmoja wa pekee asiye kua na mshirika, na hakika babu yangu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na hakika baba yangu ni kiongozi wa waumini…) kisha akataja Imamu baada ya Imamu hadi akafika kwake, akasema: (Ewe Mwenyezi Mungu fanikisha ahadi yangu na ukamilishe kazi yangu unipe nguvu na uijaze dunia haki na uadilifu kutokana na mimi…).