Kila siku Adhuhuri waumini wanaelekea katika haram ya bwana wa Mashahidi au haram ya Abulfadhil Abbasi (a.s), kwa ajili ya kushiriki katika ibada muhimu zaidi ndani ya mwezi huu mtukufu, ambayo ni ibada ya kusoma Qur’an tukufu, hufanywa ndani ya haram hizo mbili, na ambayo ni ratiba muhimu zaidi ya Ataba mbili tukufu Husseiniyya na Abbasiyya, katika mazingira tulivu yanayo mpatia mshiriki unyenyekevu katika moyo, waumini hujitokeza kwa wingi katika usomaji wa Qur’an Tartiil.
Vikao vya wasomaji wa kitabu cha Mwenyezi Mungu mtukufu katika haram tukufu ya Imamu Hussein na Abulfadhil Abbasi (a.s) vimezungukwa na maua na ujumbe mbalimbali ulio andikwa kwa nakshi katika ubao au kwa kutumia maua ya rangi, wasomaji na watafakariji wa aya tukufu kwa nyoyo zilizo jaa unyenyekevu, wanashirikiana na jopo la wasomaji wa kimataifa wanao ongoza kisomo hicho kitukufu.
Ataba mbili tukufu Husseiniyya na Abbasiyya kupitia taasisi zao zinazo husika na Qur’an, zimeandaa mazingira mazuri ya usomaji wa Qur’an, kiongozi wa Darul Qur’an ya Atabatu Husseiniyya tukufu, Shekh Hassan Mansuur amesema kua: “Kikao cha usomaji wa Qur’an kinacho fanyika katika ukumbi wa haram ya Imamu Hussein (a.s) ni moja ya vikao vinavyo hudhuriwa na watu wengi zaidi na kina mpangilio mzuri, kikao hicho huanza saa tisa hadi saa kumi Alasiri, katika kikao hicho hushiriki wasomi mahiri wa Karbala na kutoka katika mikoa mingine ya Iraq, ambapo husomwa juzuu moja kila siku”.
Naye Shekh Jawadi Nasrawiy mkuu wa Maahadi ya Qur’an ya Atabatu Abbasiyya tukufu, amesema kua: “Usomaji wa Qur’an Tartiil ni moja ya ratiba muhimu katika Maahadi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwezi ambao ni tofauti na miezi mingine, michana yake ni bora kuliko michana yote na usiku wake ni bora kuliko usiku wote, usomaji wa Qur’an unafanyika kila siku kuanzia saa kumi na moja Alasiri na husomwa juzuu moja kila siku, imeandaliwa sehemu maalumu ya kusomea Qur’an ndani ya ukumbi wa haram tukufu, na imeandaliwa misahafu mingi kwa ajili ya kuwezesha washiriki kufuatilia kisomo cha Qur’an”.