Muhammad bun Hanafiyya (a.s) anasema: Ulipo ingia usiku wa mwezi ishirini na moja, ambao ulikua usiku wa pili (tangu ajeruhiwe), baba aliwakusanya watoto wake na watu wa nyumbani kwake na akawaaga, kisha akawaambia: Mwenyezi Mungu ndiye khalifa (msimamizi) wangu kwenu naye ananitosha, ni mbora wa kutegemewa. Akawahusia kushikamana na imani na hukumu za dini iliyo fundishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).
Kisha Imamu (a.s) akazimia kwa muda, halafu akazinduka, akasema: Huyu hapa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), na Ammi yangu Hamza, na Ndugu yangu Jafari, na Maswahaba wa Mtume (s.a.w.w), wote wanasema: Fanya haraka uje kwetu hakika tumekukumbuka, kisha akazungusha macho yake kuwaangalia watu wa nyumani kwake, akasema: Nakuageni nyote kwa utukufu wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atakupeni nguvu, na atakulindeni, msimamizi wangu kwenu ni Mwenyezi Mungu, naye atosha kua msimamizi.
Kisha akasema: Wa alaikumu salamu enyi wajumbe wa Mola wangu, akasoma neno la Mwenyezi Mungu mutukufu: (Kwa mfano wa haya watende watendao) na (Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kumcha, na watendao mema). Akainamisha kichwa chake na akaacha kuugulia, akawa anamtaja sana Mwenyezi Mungu na anatamka shahada mbili, kisha akaelekea Kibla akafumba macho na akanyoosha miguu na mikono yake, akasema: Ash-hadu an laa-ilaaha illa Llaha wa Ash-hadu anna Muhammada abduhu wa rasuluhu, kisha akakata roho (a.s)..
Bibi Zainabu na Ummu Kulthum pamoja na wanawake wote wakaanza kulia kwa sauti kubwa, Waa Imamaahu!! Waa Aliyaahu!! Waa Sayyidaahu, sauti ya vilio ikawa kubwa… watu wa mji wa Kufa wakatambua kua Kiongozi wa Waumini (a.s) amefariki, wanaume kwa wanawake wakaanza kumiminika (katika nyumba yake) makundi kwa makundi, huku wakilia sana, mji wa Kufa ukajaa vilio kila mahala, ikawa kama siku aliyo kufa Mtume (s.a.w.w)..
Muhammadi bun Hanafiyya anasema: Tukamuandaa usiku, Hassan (a.s) alikua anamuosha na Hussein (a.s) anammiminia maji, na wala hakuhitaji mtu wa kumgeuza, alikua (a.s) anageuka kama anavyo hitaji muoshaji kulia na kushoto, alikua na harufu nzuri kushinda miski na ambari, kisha Hassan (a.s) akamwita dada yake Zainabu na Ummu Kulthum, akasema: Enyi dada zangu nileteeni manukato ya babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) bibi Zainabu akaenda haraka kumletea…
Kisha akamfunga katika pande tano za nguo kama alivyo amrisha (a.s), halafu wakamlaza katika kitanda (jeneza), Hassan na Hussein wakashika sehemu ya nyuma ya jeneza, wakaona sehemu ya mbele inanyanyuka bila kumuona mbebaji, walio beba sehemu ya mbele ni malaika Jibrilu na Mikaeli.. na wao (Hassan na Hussein) wakabeba sehemu ya nyuma.
Walipo fika sehemu lilipo kaburi lake, wakaona sehemu ya mbele inashushwa chini na wao (Hassan na Hussein) wakashusha, kisha Hassan (a.s) akaswalisha swala ya jeneza, akasoma takbira saba, kama alivyo ambiwa na baba yake.
Muhammad bun Hanafiyya anasema: kisha tukatikisa kitanda (jeneza) lake, tukaona udongo, kisha tukaona kaburi lililo chimbwa na mwanandani upo, na ubao ulio andikwa: (Hapa paliandaliwa na Mtume Nuhu kwa ajili ya mja mwema mtakasifu), walipo anza kumshusha katika mwanandani wa kaburi lake wakasikia sauti ikisema: Mteremsheni katika udongo mtakatifu, hakika mpenzi amemkumbuka mpenzi wake, watu wakashtushwa na sauti hiyo na wakatahayari, akazikwa kiongozi wa Waumini (a.s) kabla ya kuchomoza Alfajiri.