Mazingira ya mwezi wa Ramadhani yalikua yapekee kwa watu wa Karbala, kutokana na kufungamana kwao na ziara, hiyo ni desturi yao katika siku zote za mwaka, lakini mwezi wa Ramadhani una upekee wake, wanahistoria wanasema kua; uwanja wa haram tukufu ya malalo ya Imamu Hussein na ndugu yake Abulfadhil Abbasi (a.s), ulikua unaitwa uwanja wa mikutano ya familia za karibu na majirani kila siku baada ya futari, walikua wanaishi kana kwamba watu wote wa Karbala ni familia moja, walikua wanakutana na kufanya ibada ya ziara na ibada zingine za usiku katika mwezi wa Ramadhani, sehemu hizi tukufu na maeneo yanayo zizunguka zilikua sehemu muhimu kwa waliokua wanatafuta mazingira bora ya mwezi wa Ramadhani.
Ustadh Ali Khabbaaz ambaye ni kiongozi wa idara ya habari ya Atabatu Abbasiyya tukufu ametuelezea aliyo shuhudia na aliyo hadithiwa kuhusu mazingira hayo, amesema kua: “Hakika kufungamana kwa watu wa Karbala na dua Iftitaahi, na kuisoma au kuisikiliza wakiwa ndani ya uwanja wa haram tukufu ilikua kawaida katika mwezi wa Ramadhani, kwa kiasi hadi watoto walikua wanahifadhi dua hiyo au sehemu za dua.
Sasa hivi –inasikitisha- kufungamana na dua Iftitaahi kumepungua sana, hali kadhalika kufungamana na maeneo ya ibada na misikitini sio kama ilivyo kua katika zama zetu, zamani alikua hapatikani kijana au mtu anaye baki nyumbani baada ya futari, watu wote walikua wanaenda katika nyumba za ibada, kufungamana huko kulifasiriwa na safari za kwenda katika Ataba zingine kila baada ya siku tatu, walikwenda katika Atabatu Alawiyya au Kadhimiyya, walikua wanakutana familia kadhaa na wanasafiri kwa pamoja, jambo hili linaendelea hadi leo na umekua ni urithi wa Karbala na umeathiri jamii, na Ijumaa ya mwisho walikua wanakwenda kufanya ziara katika malalo ya Samaraa”.
Kuhusu uhusiano wa kijamii na watu kutoka nje ya Karbala, katika kuwasiliana na mazuwaru wa mikoa mingine, walio kua wakija katika malalo za Karbala kwenye minasaba ya dini, hasa katika mwezi wa Ramadhani, Ali Khabbaaz anasema kua: “Uhusiano na mazuwaru ulikua mzuri na wa kijamii zaidi, kwa sababu ya uwazi wa familia za watu wa Karbala na kupatikana kwao katika uwanja wa haram mwezi mzima wakati wa usiku, walijuana na familia nyingi zilizo kuja kufanya ziara, kwa hiyo undugu uliimarika na huduma pia zilikuwepo, kulikua na mawakibu zilizo kua zikipika na kugawa chakula kwa mazuwaru katika mwezi wa Ramadhani, ilikua ni nadra sana kumuana zaairu anakwenda kula hotelini, hivi sasa zaairu anaweza kuja na chakula chake, lakini zamani alikua anapo fika Karbala anakuta chakula tayali kimeandaliwa kwa ajili yake”.
Hakika ni utamaduni mzuri, unao onyesha mapenzi ya kweli yatokanayo na Mwenyezi Mungu mmoja wa pekee, pamoja na kuheshimu dini ya kiislamu na mafundisho yake matukufu, nayo ni mafundisho bora kushinda mafundisho ya dini zingine, mafundisho ya kujenga maelewano, na mafungamano ya kijamii, na njia za kusaidiana kijamii, na kuenzi tamaduni nzuri zisizo pingana na mafundisho ya uislamu, pia ni mafundisho bora ya kumtaja Mwenyezi Mungu mtukufu, na kuwaombea waumini heri, baraka, rehma, subira na mafanikio katika kila kitu.