Usomaji wa Qur’an ndani ya mwezi wa Ramadhani ni jambo tukufu sana, Ramadhani ni mwezi wa Qur’an, kuiangalia, kuisoma, kujifundisha, kuifundisha, kuihifadhi, kuisikiliza, kuifasiri, kuitafakari, kujikumbusha na kuienzi, kwa ajili hiyo; Maahadi ya Qur’an tawi la wanawake chini ya kitengo cha maarifa ya kiislamu na kibinadamu cha Atabatu Abbasiyya tukufu, kutokana na ratiba waliyo andika ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, wamefanya zaidi ya mahafali (100) za Qur’an ndani ya mwezi huu mtukufu, mahafali hizo zimekua ni ukamilisho wa harakati za Qur’an zinazo fanywa na wanaume.
Kiongozi wa idara ya Qur’an kitengo cha wanawake Ustadhat Manaar Jawaad Jiburi amebainisha kua: “kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: (Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’an kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi..) na kutokana na ratiba ya Qur’an yenye malengo bora iliyo andaliwa, Maahadi imefanya mahafali na vikao vya wazi vya usomaji wa Qur’ an ndani na nje ya mkoa wa Najafu na katika matawi yake yaliyopo mikoani na katika malalo na mazaru tukufu”.
Akabainisha kua: “Idadi ya mahafali na vikao vya usomaji wa Qur’an katika mkoa wa Najafu imefika (50) na katika mikoa mingine ambayo ni: (Bagdadi – Waasit – Dhiqaar – Baabil – Karbala) imefika (63).
Kuhusu vipengele muhimu vya harakati hizi za Qur’an zilizo fanywa katika misikiti au katika Husseiniyyaati na katika Atabaati tukufu na mazaru au katika nyumba za watu binafsi, Jiburi amefafanua kua: “Mahafali na vikao vya usomaji wa Qur’an vilikua na usomaji wa Tartiil, mashindano, mihadhara ya Fiqhi pamoja na usomaji wa kufundishana”.