Marjaa dini mkuu amewataka raia wa Iraq kurudisha haki zao za kisiasa, kiuchumi na kijamii, akasisitiza kua lazima anaye taka kurudisha haki yake akasirike kwa kiwango, na haki huchukuliwa na wala haipewi.
Ameyasema hayo katika khutuba ya pili ya swala ya Ijumaa iliyo swaliwa katika ukumbi wa haram tukufu ya Imamu Hussein (a.s) leo (20 Dhulqa’ada 1439h) sawa na (3 Agosti 2018m), iliyo swalishwa na Mheshimiwa Sayyid Ahmadi Swafi, ifuatayo ni nakala ya khutuba hiyo:
Mabwana na mabibi; siku za nyuma tulitaja mambo yanayo husiana na hasira, na tukaelezea matokeo mabaya yanayo sababishwa na hasira isiyo kuwa na kipimo au udhibiti, na tukataja baadhi ya mifano kuhusu jambo hilo, leo tunataja matokeo mazuri ya hasira, na je! Hasira inaweza kumsaidia mwanadamu kufikia malengo yake au haiwezi?
Kwanza hasira ni hali ya kimaumbile, imepokewa katika hadithi kua (Hana kheri asiye kasirika anapo kasirishwa), neno zuri sana (Hana kheri asiye kasirika anapo kasirishwa) hasira ni katika maumbile ya mwanadamu, mwanadamu yeyote hufikwa na hali ya kukasirika, na hasira ndio kinga yake, mtu anapo kasirika hujihami.
Mtu anapo fikwa na jambo la kumkasirisha hukasirika, lakini kama hasira itamtoa katika malengo yake na ikazuia umezo wa akili yake, mtu huyo ataingia katika wale tulio taja siku za nyuma, atapata matokeo mabaya ambayo atayajutia, lakini mtu anapo kasirika kutokana na tatizo lake binafsi, la kijamii, kiuchumi, kisiasa au kijeshi, hasira hiyo ikamtoa nyumbani kwake kwa ajili ya kwenda kutatua tatizo hilo, pia akaweza kuidhibiti hasira yake basi hasira hiyo itakua inafaa.
Hasira ndio zinazo linda mataifa, ardhi na zinazuia kunajisiwa maeneo matukufu, mwanadamu anapo kasirika na akajua kwa nini amekasirika bila shaka hasira yeke itakua na matokeo mazuri, atakua amekasirishwa na jambo maalumu na hasira zake zina lengo maalumu kuanzia mwanzo hadi mwisho, matokeo yake yatakua vipi? Mtu anaye kasirika na akaweza kumiliki hasira zake, ataweza kujieleza, ataweza kutoa madai yake na ataweza kuonyesha haki yake.
Kwa nini? –zingatieni- kwa sababu haki huchukuliwa na wala usisubiri kupewa, anaye kuibia haki yako, huyo ni mwizi wa haki na atataka aendelee kubakia na haki yako, ni wajibu kwa mwenye haki kuchukua haki yake, haki huchukuliwa, ili uweze kurudisha haki yako unatakiwa ukasirike kwa kuchukuliwa haki yako, mtu akikasirika kwa sababu ya kuchukuliwa haki yake, atakua na hoja madhubuti, madai yake yatakua wazi na hoja zote zitamlinda na hazita mkandamiza.
Kwa hiyo hasira ni jambo muhimu kwa mwanadamu, inamsaidia kujieleza, ndio! Mtu hatakiwi kukasirika kwa kila jambo, bali anatakiwa ajuwe kwa nini anakasirika? Kuna tatizo la kisiasa, kiuchumi, kijamii na tatizo hilo halitatuliwi, hadi aonyeshe hasira zake, au alalamike lakini kwa kiwango, kwa kufuata kanuni isemayo haki huchukuliwa, ni lazima kwa anaye taka kurudisha haki yake awe na uwezo wa kumiliki hasira zake, atowe hoja zenye nguvu, madai ya wazi na atumie akili, sasa linganisheni baina ya hasira tuliyo taja siku za nyuma yenye matokeo mabaya, na hasira yenye matokeo mazuri ambayo inalinda mataifa, ardhi na maeneo matukufu ambayo huwa ni matokeo ya kudhibiti hasira na kutumia akili.