Mwezi pili Rabiul Awwal mwaka 61 hijiriyya msafara wa Ahlulbait (a.s) waliokua wametekwa waelekea Yathriba (Madina), wakaanza kutembea wakiwa wapweke, huku macho ya wanawake wa familia ya Mtume (s.a.w.w) yakiwa yanabubujika machozi na kumlaani muuwaji wao pamoja na kutaja madhila waliyo fanyiwa, wakazi wa Yathriba walikua wanaenda kuomboleza na kumpa pole mama wa waislamu Ummu Salama mke wa Mtume (s.a.w.w), ambaye alikufa mwezi mmoja baada ya kuuwawa Imamu Hussein (a.s).
Imamu Zainul-Aabidina (a.s) alipofika karibu na mji wa Madina alisimamisha msafara na wakafunga hema, wanawake wa Alawiyya (watokanao na kizazi cha Imamu Ali –a.s-) wakaja wakiwa na Bishru bun Hadhlam, wakasema kumwambia Bishru:
(Ewe Bishru, Mwenyezi Mungu amrehemu baba yako hakika alikua mshairi, je wewe unaweza kusoma shairi lolote?)
Akasema: Ndio ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Bishru akaenda katika mji wa Madina, alipo fika katika nyumba ya Mtume akasoma mashairi kwa sauti ya juu huku analia:
Enyi watu wa Yathriba hakuna heshima kwenu tena *** Hussein ameuwawa mlilieni.
Mwili wake umelala Karbala *** na kichwa kimetungikwa juu ya mkuki kinazungushwa.
Watu wakamiminika katika nyumba ya Mtume wakiwa wanalia sana na wakimtaka Bishru awape taarifa zaidi, wakamzunguka na kumuuliza: kuna habari gani? (akawaambia) Ali mtoto wa Hussein na shangazi yake pamoja na dada zake wanakuja, ameniagiza nije kukuambieni ujio wao na kukuambieni walipo. Watu wakaangua kilio, na wakaondoka haraka kwenda kuipokea familia ya Mtume (s.a.w.w), vilio vikaeneo kila kona sauti za vilio vya wanawake zikawa juu walipo kutana na wanawake wa Alawiyya, na upande wawanaume pia walilia sana walipo kutana na Imamu Zainul-Aabidina (a.s), siku hiyo ilikua sawa na siku aliyo kufa Mtume (s.a.w.w).
Imamu Zainul-Aabidina (a.s) akatoa khutuba kali aliyo elezea mambo yaliyo wasibu Ahlulbait (a.s) ya kuuwawa, kudhalilishwa na kutekwa na mengineyo mengi miongoni mwa madhila makubwa, Swa’aswa’a akaomba samahani kwa Imamu kutokana na kushindwa kwao kwenda kumnusuru Hussein (a.s), Imamu akakubali udhuru wake na akaomba baba yake arehemewe.
Kisha Imamu na shangazi yake pamoja na dada zake wakiwa wamezungukwa na kundi kubwa la watu wanaolia, wakaelekea katika nyumba ya Mtume, walipo fika katika nyumba hiyo bibi Zainabu akashika frem ya mlango na akaanza kumuongelesha babu yake na kumpa pole kwa kuuwawa mjukuu wake, alisema: (Ewe babu, nakulilia kutokana na machungu ya kuuwawa kaka yangu Hussein), hapo Alawiyya wakafanya maombolezo makubwa ya kifo cha bwana wa mashahidi na wakavaa nguo nyeusi, kwa kweli ulikua msiba mzito mno.