Katika kitabu cha Kibrit Ahmaru na vinginevyo imeandikwa kua Abulfadhil Abbasi (a.s) alishirikiana na baba yake kiongozi wa waumini (a.s) katika vita ya Swifiin, na alionyesha ushujaa wa hali ya juu, alithibitisha uwezo wake pamoja na majemedari wenzake, hapo akajulikana kwa jina la simba na likawa mashuhuri.
Miongoni mwa matukio ya kishujaa aliyo fanya ni tukio la kuvamia mto wa Furat na kulifurusha jeshi la Muawiya kwenye maji, Muawiya alikua amedhibiti mto wa Furat na akaweka maelfu wa wanajeshi kulinda mto huo na kuwazuwia askari wa Imamu kiongozi wa waumini (a.s) wasichote maji, hadi wakazidiwa na kiu askari wa Imamu (a.s), ndhipo Imamu (a.s) akatoa khutuba kali na kuwahimiza waende kuvamia mto wa Furat, akachukua jukumu la kutekeleza amri hiyo mjukuu wa Mtume (s.a.w.w) Imamu Hussein (a.s), akaondoka na kundi la wapanda farasi pamoja na ndugu yake Abulfadhil Abbasi (a.s), wakaenda kuvamia mto wa Furat, wakarifurusha jeshi la Muawiya na wakachota maji, kisha wao hawakufanya kama alivyo fanya Muawiya, waliwaruhusu askari wake kuchota maji.
Abulfadhil Abbasi (a.s) katika vita ya Swifiin:
Miongoni mwa mambo ya kishujaa aliyo fanya Abulfadhil Abbasi (a.s) katika vita ya Swifiin, alitoka kupigana akiwa amevaa nikabu (ninja), watu wakamuogopa, Muawiya akamwambia Abu Sha’athaa aende kupigana naye, Abu Sha’athaa akamwambia Muawiya mimi ni sawa na wapanda farasi elfu moja huyu sio saizi yangu, nitamtumia mtoto wangu atammaliza, alikua na watoto saba.
Kila mtoto aliye kwenda kupigana na Abulfadhil Abbasi (a.s) aliuwawa, hadi akawamaliza wote, Abu Sha’athaa akakasirika sana, akasema: nitaenda kumuua mimi mwenyewe.
Kisha akaenda kupigana nae, Abulfadhil Abbasi (a.s) akampiga pigo kali akafariki na kuungana na watoto wake saba, jeshi la Muawiya lilipo ona hivyo liliogopa na kukimbia, hakuna yeyote aliye thubutu tena kupigana na Abulfadhil Abbasi, akarudi na ushindi.
Huo ni upande wa jeshi la Muawiya, amma upande wa jeshi la kiongozi wa waumini (a.s), walishangwazwa na ushujaa wake na namna alivyo pigana kwa ujasiri mkubwa, baada ya kurudi kiongozi wa waumini alimpongeza kwa ushindi huo, kisha akavua nikabu (ninja) usoni kwake akaonekana wazi kua ni mwanae Mwezi wa bani Hashim Abulfadhil Abbasi (a.s).