Imepokewa kutoka kwa Asmaa kwamba Fatuma Zaharaa (a.s) alipokaribia kufariki alimwambia Asmaa kua: (Hakika Jibrilu alimletea Mtume –wakati wa kifo chake- Kafuur kutoka peponi, akaigawa mafungu matatu matatu, mafungu matatu ya kwake, na matatu ya Ali, na matatu ya kwangu, kulikua na (dirham arubaini), kisha akasema: (Ewe Asmaa niletee manukato ya baba yangu yapo sehemu kadha na uyaweke kichwani kwangu), akachukua na kumuwekea, kisha akasema kumwambia Asmaa baada ya kutawadha kwa ajili ya swala: (Niletee manukato yangu ambayo huwa natumia na uniletee nguo yangu ya kuswalia), akavaa kisha akaswali halafu akasema: (Nisubiri kidogo halafu uniite, nikiitika sawa na nisipo itika ujue nimekwenda kwa baba yangu utume ujumbe kwa Ali).
Alipokaribia kukata roho pazia likaondolewa bibi Fatuma (a.s) alitazama kisha akasema: (Amani iwe juu ya Jibrilu, amani iwe juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, Ewe Mola pamoja na Mtume wako, ewe Mola katika radhi zako na jirani yako na nyumba yako nyumba ya amani), kisha akasema: (Huu msafara wa viumbe wa mbinguni na huyu ni Jibrilu na huyu Mtume wa Mwenyezi Mungu anasema: njoo ewe mwanangu kilichopo mbele yako ni kheri kwako) akafunua macho yake kisha akasema: (Amani iwe juu yako ewe mtoa roho fanya haraka wala usiniadhibu), akasema: (kwa utukufu wako hauwendi motoni katu) kisha akafunika macho yake na akanyoosha mikono na miguu yake, Asmaa akamwita hakumwitikia, akamfunua nguo usoni kwake akakuta amesha aga dunia. Hassan na Hussein wakaingia wakakuta mama yao amesha fariki, wakamuuliza Asmaa, kitu gani kinamlaza mama yetu katika mda kama huu? Asmaa akawaambia: Enyi watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu mama yenu hajalala bali amesha aga dunia.
Hassani amwinamia mama yake huku anambusu na kusema: (Ewe mama yangu niongeleshe kabla roho yangu haijanitoka), na Husseini akabusu miguu ya mama yake huku anasema: (mimi ni mwano Husseini niongeleshe kabla moyo haujatoka na kufariki).
Asmaa akawaambia: Enyi watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, nendeni kwa baba yenu Ali mkamwambie kifo cha mama yenu, wakatoka hadi walipofika karibu na msikiti wakapaza sauti za kulia, maswahaba wakawakimbilia na kuwauliza kwa nini wanalia, wakasema: (Mama yetu Fatuma (a.s) amesha fariki).
Imamu Ali (a.s) akajipiga usoni kwake huku anasema (nani wa kuomboleza ewe binti wa Muhammad).