Mwezi 15 Rajabu ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha bibi Zainabu Alkubra (a.s), aliye lelewa katika nyumba ya elimu na maarifa, nyumba ya wahyi na utume, ameishi katika madrasa ya Utume na Uimamu, na akahitimu madrasa zote mbili, amelelewa na Mtume Muhammad (s.a.w.w) pamoja na wasii wake Ali bun Abu Twalib (a.s) na Ummu Abiha Fatuma Zaharaa (a.s) mbora wa wanawake wa duniani na Hassan na Hussein (a.s) mabwana wa vijana wa peponi, na mwenye kuhitimu katika madrasa hizo, anaweza kuwa mfano kwa wanawake wema.
Alikua (a.s) mfano bora kwa kujisitiri, Yahaya Maaziniy anasema kua: Nilikua jirani na kiongozi wa waislamu (a.s) katika mji wa Madina kwa miaka mingi, tena karibu na nyuma aliyokua anaishi binti yake Zainabu, sikupata kumuona kwa sura wala kusikia sauti yake, alikua anapotaka kwenda kumtembelea babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) anakwenda usiku akiwa Hassan kulia kwake na Hussein kushoto kwake na kiongozi wa waumini mbele yake, wanapo karibia kaburi tukufu, anawatangulia kiongozi wa waumini (a.s), anakwenda kupunguza mwanga wa taa (kandili), safari moja Hassan akamuuliza kuhusu kitendo hicho, akasema: naogopa watu wasimwangalie dada yako Zainabu, Imamu Hussein (a.s) alikua anapo tembelewa na Zainabu anasimama kwa kumuheshimu, na anamkaribisha akae sehemu aliyokua amekaa yeye.
Hali kadhalika bibi Zainabu (a.s) alikua sawasawa na mama yake Swidiiqah Zaharaa (a.s) katika kufanya ibada, kuswali tahajudi na kufanya dhikri, alikua mwingi wa kufunga, mwingi wa kuswali, mwingi wa kusoma dua na toba, sehemu kubwa ya usiku wake aliitumia kwa kuswali tahajudi na kusoma Quráni, hakuacha kufanya ibada hizo hata katika usiku mgumu Zaidi kwake, usiku wa mwezi kumi na moja Muharam. Kutoka kwa Fadhil Naainiy Burjudiy anasema: Hussein (a.s) alipo muaga dada yake kwa mara ya mwisho alimwambia: Ewe dada yangu usinisahau katika sunna zako za usiku.
Bibi Zainabu (a.s) alishuhudia mauwaji yote yaliyo fanyika katika ardhi ya Karbala, aliona jinsi walivyo uwawa watoto wake, kaka yake, na mwezi wa bani Hashim. Yeye aliendelea kufanya subira na kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa yote yaliyo fanyika, nafasi yake (a.s) inaonekana katika kusimamia wanawake na watoto, mchango wake ulionekana sehemu nyingi.
Bibi Zainabu (a.s) alifariki mwezi 15 Rajabu katika mji wa Damaskas Sham mwaka wa 62h kwa kauli sahihi, akazikwa pembezoni mwa mji wa Damaskas, katika kitongoji kinacho itwa Raawiyah, amejengewa mazaru inayo endana na utukufu wake. Na kuna kauli kuwa alizikwa Misri, huko pia kajengewa Maqaam ambayo watu huizuru na kutabaruku.