Shekhe wa Mashekhe wa Bakdashiyya duniani kutoka Albaniya Mtukufu Mundi amesema kua: ameona Iraq imeendelea na kunawirika kama alivyo ona sehemu hii, akiashiria malalo ya Imamu Hussein (a.s).
Ameyasema hayo katika hafla ya kufunga kongamano la Rabiu Shahada ya awamu ya kumi na tano, iliyo fanyika alasiri ya Jumamosi (7 Shabani 1440h) sawa na (13 April 2019m) katika ukumbi wa haram ya Imamu Hussein (a.s) lililo fanyika chini ya kauli mbiu isemayo: (Imamu Hussein –a.s- ni mnara wa umma na suluhisho madhubuti).
Akasema: “Ndugu zangu watukufu kwanza nataka kuushukuru uongozi mkuu wa Ataba mbili tukufu Husseiniyya na Abbasiyya, na ninatoa salamu kwa wanachuoni wa taifa hili na wanachuoni waliokuja kutoka nchi mbalimbali nawatakia amani na afya njema”.
Akaongeza kua: “Nina furaha kubwa mimi kama Shekhe wa Mashekhe wa Bakdashiyya duniani ninaye fuata mwenendo wa Ahlulbait (a.s), nawashukuru raia wote wa Iraq, hii ni mara ya pili kuja Iraq, nimeikuta imeendelea na imenawirika kama ilivyo nawirika sehemu hii ambayo imeongezeka kunawirika kutokana na nuru ya nyuso zenu tukufu”.
Akabainisha kua: “Tutabaki katika mwenendo wa wanachuoni wetu na walimu watukufu na nyoyo zetu zitaendelea kuwapenda Ahlulbait (a.s) wao ndio kiigizo chetu, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, mapenzi yetu na kushikamana nao vitaongezeka, hakika twariqa ya Bakdashiyya ya kisufi daima itakua njia ya kusambaza mapenzi na amani kote duniani, sisi Albania tunaishi kwa amani na utulivu na ndugu zetu wa dini zingine, sote kwa pamoja tunatangaza amani, watu wengi wa Balkani wanaona kua Dini ya Uislamu ndio njia nzuri ya kuwafikisha katika Amani, mapenzi na ubinaadamu”.