Ukumbi wa Sayyid Auswiyaa (a.s) katika Atabatu Husseiniyya tukufu umeshuhudia kikao cha kufunga mikutano ya wanawake ya kongamano la kitamaduni na kimataifa Rabiu Shahada ya kumi na tano, na kuhudhuriwa na wanawake wengi kutoka ndani na nje ya Iraq.
Kikao cha ufungaji kilikua na vipengele vingi, miongoni mwa vipengele hivyo ni; kupokea ujumbe kutoka kwa kamati ya maandalizi, ulio wasilishwa na Mhandisi Sara Muhammad Ali, amewashukuru watu wote walio shiriki katika kongamano hili, akawaomba waendelee kushirikiana, na wajitokeze kwa wingi zaidi katika kongamano la mwaka kesho.
Ukafuata ujumbe wa bibi Bushra Kinani kiongozi wa idara ya shule za Alkafeel za wasichana ambazo zipo chini ya Atabatu Abbasiyya tukufu, akasema kua: “Tumeishi siku tatu tukinusa harufu nzuri ya kuzaliwa kwa watu watakatifu katika mwezi wa kheri wa Shabani, jambo tukufu ni kukutana kwetu kwa mjukuu wa Mtume Imamu Hussein (a.s), tukiimba kwa kumsifu na kusikiliza mafundisho matukufu, kipindi cha Rabiu Shahada ya kumi na tano nyoyo zetu zimekua zikikariri kuwa Hussein ndio mnara wa Umma na suluhisho madhubuti, baada ya bani Umayya kuleta giza”.
Akasisitiza kua: “Jambo tukufu ni kukutana wakina mama wa sekta ya habari na viongozi wa kijamii, kwa aili ya kujadili maendeleo ya wanawake pamoja na mustakbali wa mwanamke wa kiislamu wa zama hizi”.
Akamaliza kwa kusema: “Tunawashukuru sana walio fanikisha jambo hili, na kupata fursa ya kuzienzi kalamu za waandishi, na kuujulisha ulimwengu kua dunia haitaishi bila Zainabu na kaka yake Hussein (a.s)”.
Ukafuata ujumbe wa wageni washiriki ulio wasilishwa na bibi Fatuma Abdullahi Ali kutoka Komoro, akasema kua ushiriki huu imetokana na mawasiliano endelevu baina yao katika mambo muhimu ya dini, likiwemo kongamano hili la Rabiu Shahada, sambamba na kutambua majukumu tuliyo nayo katika makongamano ya aina hii, ukizingatia kua mwanamke ndio nusu ya jamii na sababu kubwa ya maendeleo”.
Mashairi yalikua na nafasi maalumu katika hafla hii, mshairi bibi Fatuma Zaharaa Zaahidi kutoka chuo kikuu cha Bagdad/ kitivo cha famasiya alikonga nyoyo za wahudhuriaji kwa kuimba kaswida nzuri iliyo taja sifa za Imamu Hussein (a.s), huku mwana habari Riyana Jamali Ridhwa akafanya darasa mjadala (nadwa) iliyo zungumzia: (Mifumo ya mawasiliano na matokeo yake kijamii).
Mwisho kabisa wakatangazwa washindi watatu wa shindano la kutoa kisa kifupi kuhusu (Mchango wa mwanamke katika kumnusuru wasii wa tatu) na kupewa zawadi, nao ni:
Mshindi wa tatu: Kisa cha sehemu iliyo kosekana katika kitabu cha Maryam Khafaji.
Mshindi wa pili: Kisa cha Mwezi wa Karbala katika kitabu cha Rajaa Baitwaar.
Mshindi wa kwanza: Kisa cha risasi laini katika kitabu cha Ruqayya Taaji.
Baada ya hapo washiriki wote wa shindano wakapewa vyeti vya ushiriki pamoja na vidani.