Usiku wa nusu ya mwezi wa Ramadhani mwaka wa tatu hijiriyya, mji wa Madina uliangaziwa na nuru ya kuzaliwa Imamu Hassan Almujtaba (a.s), katika usiku huo nyumba ya Utume katika mji wa Madina ilipata taarifa ya kuzaliwa kwa mjukuu wa kwanza, ikawa furaha kubwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), akaenda katika nyumba ya Zaharaa (a.s) kumpa pongezi, alipo fika katika nyumba ya Zaharaa (a.s) akapata wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu mtukufu, ukimwambia kua Mwenyezi Mungu amempa jina la (Hassan) mototo huyo.
Hivyo jina lake ni Imamu Abu Muhammad Hassan bun Ali bun Abu Twalib Almujtaba, Imamu wa pili katika maimamu wa nyumba ya Ahlulbait (a.s) na mmoja wa mabwana wa vijana wa peponi, mmoja wa watu wanne aliotoka nao Mtume kwenda kuapizana na manaswara wa Najrani, pia ni miongoni mwa watakasifu walio takaswa na Mwenyezi Mungu, pia yeye ni katika Qurba ambao Mwenyezi Mungu mtukufu ameamrisha tuwapende, ni mmoja wa vizito viwili ambavyo atakaye shikamana navyo ataongoka na kuokoka na atakaye viacha atapotea na kuangamia.
Alilelewa na babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), akasoma elimu na tabia zake, akaendelea kua karibu na babu yake hadi alipo chukuliwa na Mwenyezi Mungu baada ya kumrithisha adabu na haiba yake, na kumwandaa kwa uimamu baada ya baba yake kiongozi wa waumini, hakika alifanana sana na babu yake pamoja na baba yake, waumini walikua wanapo mkumbuka Mtume wanamwangalia yeye, walimpenda na kumtukuza, alikua kimbilio lao kuu wanapo tofautiana katika jambo lolote, hususan baada ya umma kuanza kuingiliwa na hadithi za uzushi pamoja na mambo ambayo hayakuwepo zamani.