Katika siku kama ya leo mwezi nane Muharam 61h Abulfadhil Abbasi (a.s) aliumizwa sana alipoona watoto wa ndugu yake na watu wa nyumba ya Mtume (a.s) wanalia kutokana na kiu kali waliyo nayo.
Imeandikwa kua; kiu kilipo mzidia Imamu Hussein na wafuasi wake, alimwita ndugu yake Abbasi (a.s), akampa wapanda farasi thelathini na watembea kwa miguu ishirini wakiwa na viriba ishirini katikati ya usiku wakaenda hadi karibu na mto wa Furaat, wakiwa wametanguliwa na Naafii bun Hilali Almuraadi aliyekua miongoni mwa wafuasi wakubwa wa Imamu Hussein (a.s), wakakutana na Omari bun Hajjaaj Zubaidiy aliyekua kapewa jukumu la kulinda mto wa Furaat, maluuni huyo akasema kumwambia Naafii: Kitu gani kinakuleta? Akasema: Tumekuja kunywa maji mliyo tuharamishia na kutuzuwia. Akasema: kunywa. Akamwambia: Ninywe na Hussein akiwa na kiu? Yeye na wafuasi wake? Akasema: hakuna njia ya kumpa maji yeye na wafuasi wake, tumewekwa hapa kuzuwia wasipate maji.
Wafuasi wa Imamu Hussein (a.s) hawakusikiliza maneno yake, walivamia mto na kuchota maji, Omari bun Hajjaaj na watu wake wakataka kuwazuwia, ndipo akaingia kamanda wa Karbala Abulfadhil Abbasi (a.s) na Naafii bun Hilali, wakapigana vita kali lakini hakuna aliye kufa pande zote mbili, wafuasi wa Imamu wakarudi kwenye mahema yao wakiwa wamejaza maji viriba vyao chini ya uangalizi wa Abulfadhil Abbasi (a.s).
Kuanzia siku hiyo Abulfadhil Abbasi (a.s) akapewa jina la mnyweshaji (Saqaa), nalo ni jina tukufu na maarufu zaidi kwake.