Muhimu na hivi sasa.. nakala ya tamko la Marjaa Dini mkuu kuhusu hali tete ya taifa la Iraq

Maoni katika picha
Mwakilishi wa Marjaa Dini mkuu katika khutuba ya Ijumaa ya leo (26 Safar 1441h) sawa na (25 Oktoba 2019m) ndani ya haram tukufu ya Imamu Hussein (a.s), amesoma tamko la Marjaa Dini mkuu kutoka mji mtukufu wa Najafu.

Mheshimiwa Shekh Abdulmahdi Karbalai amesema kua:

Mabwana na mbibi.. nakusomeeni nakala iliyo tufikia kutoka ofisi ya Mheshimiwa Ayatullah Sayyid Sistani:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu

Taifa letu la Iraq linapitia wakati mgumu, wakati ambao raia wanafanya maandamano kila siku katika mji mkuu wa Bagdad na mikoa mingine, tunatoa wito kwa ndugu zetu waandamanaji na vyombo vya ulinzi na usalama, kila mmoja awe mlinzi wa amani, ajizuwie kufanya uhalifu na kutumia nguvu.

Tunawaomba waandamanaji wajizuwie kuwachokoza askari kwa namna yeyote ile, pia tunawaomba wasiharibu mali za raia na mali za umma wala wasishambulie majengo ya serikali pamoja na majengo ya watu binafsi.

Kuwachokoza askari kwa kuwapiga mawe au kuwarushia vitu vyovyote na kushambulia mali za umma na binafsi kwa kuchoma, kupora au kusababisha uharibifu wowote, mambo hayo hayakubaliki kisheria, yanapingana na maandamano ya amani na yanakua kikwazo cha kutofanyiwa kazi madai ya waandamanaji pia inabidi watu wanao fanya hayo wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Tunavikumbusha vyombo vya ulinzi na usalama kua maandamano ya amani ni haki ya kila raia aliyo pewa na katiba, jukumu lao ni kulinda usalama wa waandamanaji katika viwanja vya wazi, barabarani pamoja na kila sehemu walipo waandamanaji, mnatakiwa kujizuwia kutumia nguvu kwa aina yeyote mnapo amiliana na waandamanaji, maadamu hawafanyi vurugu wala hawashambulii mali za umma.

Marjaa Dini anasisitiza maandamano yawe ya amani yasiyo kua na matumizi ya nguvu, sio kutoshambuliana baina ya waandamanaji na askari tu, bali kipaombele cha kila mtu kiwe ni mustakbali wa taifa hili lenye mitihani mingi, linalo hofiwa kudumbukia kwenye dimbwi la vurugu, kawaida ya vurugu huleta uharibifu, jambo ambalo hufungua milango ya kuingiliwa na mikono ya nje, mara nyingi matokea yake hua mabaya, kama ilivyo tokea katika mataifa mengine, wamejikuta hawana utulivu kwa miaka mingi.

Hakika islahi ya kweli na mabadiliko yanayo takiwa katika idara za serikali yanatakiwa kutafutwa kwa njia za amani, itawezekana iwapo wairaq wakishikamana na kusimama mstari mmoja katika kudai mambo maalum.

Kuna mambo mengi ambayo wairaq wanakubaliana na wamekua wakiyadai kwa muda mrefu, miongoni mwa mambo hayo ni kupambana na ufisadi, kwa kutumia njia za wazi na kurudisha mali za raia, pamoja na kufanya haki katika kugawa mali za taifa na kuondoa vipengele vinavyo wapa haki zaidi viongozi wakubwa na wabunge, sambamba na kutumia kanuni za wazi katika kutoa ajira serikalini wala sio kwa kujuana na upendeleo, pamoja na kuhakikisha siraha zote zinakua chini ya udhibiti wa serikali, na kuzuwia kuingiliwa na mataifa ya nje, na kuunda sheria bora za uchaguzi zitakazo wapa raia matumaini ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki utakao wavutia kushiriki.

Kwa mara nyingine tena tunawaomba waandamanaji watukufu wadhibiti hasira walizo nazo zinazo tokana na mazingira magumu na ufisadi, wasiwashambulie askari au mali za umma na binafsi.

Hakika skari ni baba zenu au ndugu zenu au watoto wenu na wamefanya kazi kubwa ya kukulindeni, wamepigana na magaidi wa Daesh na wengineo waliotaka kukufanyieni mabaya, na leo wanatekeleza majukumu yao ya kulinda mali za umma, mnatakiwa kuwaheshimu na kuwanyenyekea, msiruhusu watu wenye nia mbaya wakaingia katikati yenu, wakatumia maandmano yenu kuwashambulia askari wetu watukufu, au kushambulia majengo ya serikali na mali za raia.

Pia tunavikumbusha vyombo vya ulinzi na usalama kua; waandamanaji ni baba zenu, ndugu zenu na watoto wenu, wanadai haki zao na kutetea mustakbali wa taifa lao, muwachukulie kwa upole na huruma.

Taarifa ya uchunguzi iliyo tangazwa, inayotaja maafa na uharibifu uliotokea katika mandamano haijafikia malengo tarajiwa, haijataja kwa uwazi mambo yote yaliyo tokea, ni muhimu kuunda kamati huru itakayo fanya uchunguzi katika jambo hili, na kulitangazia taifa kwa uwazi matokeo ya uchunguzi wao.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu mtukufu ailinde Iraq na ria wake kutokana na shari za watu waovu na vitimbi vya maadui hakika yeye ni mwingi wa rehema mwenye kurehemu.
Maoni ya wasomaji
Hakuna maoni
Kuweka maoni
Jina:
Nchi:
Barua pepe:
Kushiriki: