Nyumba ya uteme na wafuasi wao wote na wapenzi wao iliingia furaha mwezi kumi Rabiul-Aakhar mwaka wa (232h) katika mji wa Madina kwa kuzaliwa nuru miongoni mwa nuru za Muhammadiyya, alizaliwa mtukufu Imamu Hassan Askariy na kupokelewa na baba yake Imamu Ali Haadi (a.s) kwa shangwe na furaha kubwa, kwa sababu ni muendelezo wa utume na mrithi wa elimu za mitume na mawasii, akamfanyia taratibu za mtoto kama alivyo kua anafanya Mtume (s.a.w.w) alipo zaliwa Hassan na Hussein (a.s), akamuadhinia katika sikio la kulia na akamsomea Iqama kwenye sikio la kushoto, siku ya saba akamnyoa nywele na akatoa sadaka ya fedha kwa uzito wa nywele hizo na kumfanyia hakika kisha akampa jina la Hassan na kuniya ya (Abu Muhammad), akampa malezi bora kabisa, chini ya mafunzo na usimamizi wa Mwenyezi Mungu kama Mtume alivyo simamia malezi ya Ali (a.s), akapata elimu kubwa na hekima akiwa bado mdogo (a.s).
Imamu Askariy ni Imamu wa kumi na moja katika Maimamu wa nyumba ya Mtume (a.s), jina lake ni Hassan bun Ali bun Muhammad bun Ali bun Mussa bun Jafari bun Muhammad bun Ali bun Hussein bun Ali bun Abu Twalib (a.s).
Mama yake anaitwa (Hudithi) pia inasemekana kua anaitwa (Salilu) na wengine wanasema anaitwa Juddah, alikua mama mchamungu sana, yatosha katika kueleza utukufu wake maneno aliyo sema Imamu Haadi (a.s): (Salilu amesitirika na mapungufu na machafu).
Imamu Hassan Zakiy alishika madaraka ya Uimamu baada ya kifo cha baba yake Imamu Haadi (a.s) mwaka wa 254h akiwa na umri wa miaka 22, aliongoza kwa muda wa miaka sita na miezi kadhaa, ulidiriki utawala wa Mu’taz Abbasiy kisha utawala wa Muhtada miezi kumi na moja, halafu utawala wa Mu’tamad mtoto wa Mutawakkil, na alifariki Imamu Askariy (a.s) katika utawala wa huyo kiongozi wa mwisho, aliishi na baba yake miaka ishirini na tatu.
Amekua mashuhuri zaidi kwa laqabu ya Askariy kutokana na mahala nyumba ya baba yake ilipokua, palikua panaitwa (Askariy) ulikua mji fakiri ukafanywa kuwa makazi ya askari, kazi kubwa iliyo fanywa na Imamu Hassan Askariy (a.s) aliasisi na kuandaa mazingira ya ghaiba ndogo na kubwa.
Imamu Askariy (a.s) alikua sawa na baba zake, alikua mwalimu wa wanachuoni na kiigizo chema kwa watafuta haki, alikua mwanasiasa mahiri wa kupigiwa mfano, watu wote walimpenda na kumuheshimu hadi maadui zake walikiri utukufu wake.
Miongoni mwa sifa za Imamu Askariy (a.s) alikua mweusi mwenye umbo na sura nzuri, alikua na haiba nzuri mbele ya kila mtu, alikua mtaratibu, mkarimu na mchamungu, pete yake ilikua imeandikwa: (Subhana man lau maqaaliidu samawaati wal-ardhu) au (Ana lilahi shahiidu) au (Allahu shahiidu). Hirizi yake ilikua: (Yaa uddatii inda shiddatii wa yaa ghiyathi inda kurbatii wa yaa mu-unisii inda wahdatii, uhrusni biainika latii laa tanamu wakfini birukunika alladhii laa yuraamu).